عن عُمَرَ بْنِ الْخَطَّابِ – رضي الله عنه - قَالَ: بَيْنَمَا نَحْنُ عِنْدَ رَسُولِ اللهِ ﷺ ذَاتَ يَوْمٍ، إِذْ طَلَعَ عَلَيْنَا رَجُلٌ شَدِيدُ بَيَاضِ الثِّيَابِ، شَدِيدُ سَوَادِ الشَّعَرِ، لَا يُرَى عَلَيْهِ أَثَرُ السَّفَرِ، وَلَا يَعْرِفُهُ مِنَّا أَحَدٌ،حَتَّى جَلَسَ إِلَى النَّبِيِّ ﷺ، فَأَسْنَدَ رُكْبَتَيْهِ إِلَى رُكْبَتَيْهِ، وَوَضَعَ كَفَّيْهِ عَلَى فَخِذَيْهِ، وَقَالَ: يَا مُحَمَّدُ، أَخْبِرْنِي عَنِ الْإِسْلَامِ، فَقَالَ رَسُولُ اللهِ ﷺ: «الْإِسْلَامُ أَنْ تَشْهَدَ أَنْ لَا إِلَهَ إِلَّا اللهُ، وَأَنَّ مُحَمَّدًا رَسُولُ اللهِ ﷺ،وَتُقِيمَ الصَّلَاةَ، وَتُؤْتِيَ الزَّكَاةَ،وَتَصُومَ رَمَضَانَ، وَتَحُجَّ الْبَيْتَ إِنِ اسْتَطَعْتَ إِلَيْهِ سَبِيلًا»، قَالَ: صَدَقْتَ، قَالَ: فَعَجِبْنَا لَهُ يَسْأَلُهُ، وَيُصَدِّقُهُ،قَالَ: فَأَخْبِرْنِي عَنِ الْإِيمَانِ، قَالَ: «أَنْ تُؤْمِنَ بِاللهِ، وَمَلَائِكَتِهِ، وَكُتُبِهِ، وَرُسُلِهِ، وَالْيَوْمِ الْآخِرِ، وَتُؤْمِنَ بِالْقَدَرِ خَيْرِهِ وَشَرِّهِ»، قَالَ: صَدَقْتَ، قَالَ: فَأَخْبِرْنِي عَنِ الْإِحْسَانِ، قَالَ: «أَنْ تَعْبُدَ اللهَ كَأَنَّكَ تَرَاهُ، فَإِنْ لَمْ تَكُنْ تَرَاهُ فَإِنَّهُ يَرَاكَ»، قَالَ: فَأَخْبِرْنِي عَنِ السَّاعَةِ، قَالَ: «مَا الْمَسْؤولُ عَنْهَا بِأَعْلَمَ مِنَ السَّائِلِ»قَالَ: فَأَخْبِرْنِي عَنْ أَمَارَتِهَا، قَالَ: «أَنْ تَلِدَ الْأَمَةُ رَبَّتَهَا، وَأَنْ تَرَى الْحُفَاةَ الْعُرَاةَ الْعَالَةَ رِعَاءَ الشَّاءِ يَتَطَاوَلُونَ فِي الْبُنْيَانِ»،قَالَ: ثُمَّ انْطَلَقَ فَلَبِثْتُ مَلِيًّا، ثُمَّ قَالَ لِي: «يَا عُمَرُ أَتَدْرِي مَنِ السَّائِلُ؟» قُلْتُ: اللهُ وَرَسُولُهُ أَعْلَمُ، قَالَ: «فَإِنَّهُ جِبْرِيلُ أَتَاكُمْ يُعَلِّمُكُمْ دِينَكُمْ». رواه مسلم.



Kutoka kwa Umar bin Al-Khattab – Mwenyezi Mungu amuwiye radhi –amesimulia kuwa:

siku moja tulikuwa tumekaa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Rehma na amani ziwe juu yake) ghafla alitokea mtu mwenye mavazi meupe mno, mwenye nywele nyeusi sana, hana athari yoyote safari ndefu, na hakuna kati yetu aliyemfahamu.Alisogea na kukaa karibu na Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake) akiegemeza magoti yake juu ya magoti yake na akaweka mikono kwenye mapaja yake.Kisha akasema: Ewe Muhammad nieleze kuhusu Uislamu.Akasema Mtume wa Mwenyezi Mungu Rehma na Amani zimshukie: “Uislamu ni kushuhudia ya kwamba hapana Mola anaeabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu mmoja.Na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, Kusimamisha Sala.Kutoa zaka.Na kufunga mwezi wa Ramadhani.Na kuhiji kwenye Nyumba tukufu ikiwa mnaweza kuifikia.”Mtu yule akasema: umepatia. Tukamshangaa mtu yule anamuuliza kisha anamsadikisha.Kisha akasema mtu yule: Basi niambie kuhusu Imani. Mtume Akasema: Imani ni Kumuamini Mwenyezi Mungu.Na Malaika wake.Na vitabu vyake.Na Mitume wake.siku ya mwisho.Na kuamini makadirio yake, ya kheri au shari.” Mtu yule akasema: Umesema kweli.Kisha akasema: “Basi nielezee kuhusu Ihsani(wema/ufanisi)” Akasema Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake):ni Kumuabudu Mwenyezi Mungu kana kwamba unamuona, na ikiwa humuoni, basi Yeye anakuona.Akasema mtu yule: Basi nielezee kuhusu Kiyama).” Mtume Akasema: anaeulizwa si mjuzi zaidi kuliko muulizaji. Akasema mtu yule: Basi nielezee ishara zake, Mtume akasema: “ni mjakazi atakapomzaa bosi wake,Na kuwaona wasio na viatu, walio uchi, wachungaji wa kondoo wakishindana kujenga majumba ya kifahari.Msimulizi anasema: Kisha mtu huyo akaondoka, nikatulia muda kidogo, kisha Mtume akaniambia: Omar, umemjua ni nani muulizaji? Nikasema: “Mwenyezi Mungu na Mtume wake ndio wanajua zaidi.” Akasema: Ni Malaika Jibril amekuja kuwafundisheni dini yenu.)

Hadithi hii ni miongoni mwa misingi mikubwa iliyobainisha na kuikusanya daraja za dini, na kwa ajili hiyo Al-Qadi Iyad akasema: “Hii ni Hadithi kubwa inayojumuisha kazi zote za matendo yanayoonekana na ya yasiyoonekana, na Elimu yote ya kisheria inapatikana katika hadithi hii

Omar- Radhi za mwenyezi mungu zimshukie- anasema kwamba wao:

  1. Walipokuwa wamekaa pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu akatokea mtu mmoja mwenye sura ya ajabu. Ni kijana mwenye nywele nyeusi sana, na si miongoni mwa maswahaba mashuhuri wa Mtume, Rehema na amani ziwe juu yake, Haionekani kuwa yeye ni msafiri, kwani dalili za safari hazionekani kwake, kama vile kichwa kuchafuka na vumbi la uso na nguo.

  2. Kisha mtu huyu akaingia kwenye duara la watu mpaka akakaa mbele ya Mtume akashikanisha magoti yake kwenye magoti ya Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake) na kuweka viganja vyake juu ya mapaja yake. Tayari kwa kutafuta Elimu kwa unyenyekevu kwa Mtume, amani iwe juu yake, katika kikao hicho.

  3. Kisha akasema: Ewe Muhammad, niambie kuhusu Uislamu. na alisema: Ewe Muhammad! Kuwajulisha kuwa yeye ni Bedui; kwani wao ndio waliokuwa wakimuita Mtume, Rehema na amani ziwe juu yake, kwa jina lake tu. Kwa vile hawakuwa na elimu na adabu kama za Maswahaba katika Muhajiri na Ansari ambao walisikia amri za Mwenyezi Mungu Mtukufu na wakazitekeleza pale Mwenyezi Mungu aliposema: “Msiichukulie dua ya Mtume baina yenu kuwa ni dua ya nyinyi kwa nyinyi.” (An- Nur: 63). yaani: Msimuite kama mnavyoitana, yaani Usiseme: Ewe Muhammad, bali sema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu.[1]

  4.  Mtume Rehma na Amani zimshukie akamjibu kuhusu Uislamu, ya kwamba Uislamu umeegemezwa juu ya nguzo tano mashuhuri, ambazo ya kwanza ni: kushuhudia kwamba hapana Mwenyezi Mungu Anaeabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu mmoja; Neno hilo ni tamko la kumpwekesha Mwenyezi Mungu ambalo Mwenyezi Mungu aliwatuma nalo manabii na mitume wote, ambalo ni lazima kutamka kwa ulimi, na kukiri moyoni, na kutenda kwa viungo vyake matendo yanayoendana na imani hiyo; na asiabudiwe yeyote ila Mwenyezi Mungu, wala asimuogope yeyote isipokuwa Yeye tu, wala asiombe mwengine, na hampendi yeyote kama anavyompenda  Mwenyezi Mungu, na haweki nadhiri matumaini kwa yeyote sipokuwa yeye, na ibada nyenginezo anazifanya kwa ajili yake tu, na kuwa na yakini kwamba Yeye ndiye mwenye kudhuru na mwenye kunufaisha, kwamba hakuna yeyote mwenye manufaa au madhara kwa mja isipokuwa kwa idhini yake, yeye ndiye anaeabudiwa kwa haki, na kinyume na yeye ni uongo.

  5. Katika sharti la neno la tauhidi (kumpwekesha Mwenyezi Mungu) ni kumuamini Mtume wake (Rehma na amani ziwe juu yake), kwa yale aliyokuja nayo, na kuamini kwamba ametumwa na Mola wake Mlezi, na kusadikisha aliyoyaleta kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na hilo lahitaji kuamini aliyoyafanya kuwa sheria, na kufuata aliyoyaamrisha, na kuepuka aliyoyakataza, na kumtukuza, na kumuunga mkono, na kumtetea, na kupigania dini pamoja naye.

  6. Nguzo ya pili ya Uislamu: kusimamisha swala ambayo ni kuisimamisha kwa namna inayostahiki, baada ya kutimiza masharti na kutekeleza nguzo, pia kuwa mnyenyekevu katika swala na kuhisi utukufu wa Mwenyezi Mungu. Mwenye nguvu ndani yake, na ndio maana hakusema: “Na tekelezeni Swala.”

  7. Nguzo ya tatu: kutoa zaka, ambayo ni wajibu kwa mtu mwenye mali ambayo Mwenyezi Mungu amempatia, kwa mujibu wa maelezo ya halali ambayo Sheria tukufu imebainisha. Hivyo basi mtu anatoa zaka yake kutokana na wema wake, akiamini kuwa ni wajibu kwake, na akitarjia ujira kwa Mwenyezi Mungu, wala hachagui mali iliyombaya na kuitoa kwa ajili ya zaka, bali anatanguliza radhi na malipo ya Mwenyezi Mungu katika mali yake. 

  8. Nguzo ya nne ya Uislamu ni kufunga mwezi wa ramadhani kwa kujiepusha na mambo yanayofunguza saumu kama vile chakula, vinywaji na kujamiiana katika mchana wa mwezi wa Ramadhani, kuanzia alfajiri hadi kuchwa kwa jua, kama ilivyo katika vitabu vya sheria, muumini hufunga, na hutaraji thawabu, wala hafungi kwa kulazimishwa. 

  9. Kisha nguzo ya tano: kuhiji kwenye Nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu iliyoko Makka, na ibada nyenginezo, zenye hukumu maalumu, na ibada hiyo ni wajibu mara moja katika maisha, kwa sharti kwamba mtu awe ana uwezo wa kimwili na kifedha.

Ni vyema kutambua kwamba aliunganisha katika ufafanuzi wa Uislamu miongoni mwa nguzo zake tano ulizojengwa juu yake, kama ilivyo katika hadithi ya Abdullah bin Omar, Mwenyezi Mungu awawie radhi, amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu Alisema: “Uislamu umejengwa juu ya nguzo tano, kushuhudia kuwa hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu na Mwingi wa Rehema.” kuswali, kutoa zaka, kuhiji Nyumba na kufunga Ramadhani”

Hii haimaanishi kuwa Uislamu umewekewa mipaka kwenye ibada hizo tu, bali ni nguzo zake ambazo uislamu hauwezi kuimarika pasipo nguzo hizo, na ibada nyingine zote ni nyongeza za jengo hilo, ambalo hasara yake inaathiri jengo hilo na uhai wake, tofauti na nguzo ambazo, ikiwa zimepotea, jengo huanguka mahali pa kwanza.

10.  Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake) alipomaliza jibu lake, yule mtu akamwambia: “Umesema kweli.” Maswahaba walishangaa ni vipi atamuuliza juu ya jambo fulani kisha kulithibitisha jibu lenyewe; bila shaka muulizaji anayo Elimu ya kutosha juu ya hilo analouliza na sio kuwa hajui kabisa. 

11.  Kisha akamuuliza kuhusu Imani ambayo ni daraja ya pili ya Dini baada ya Uislamu, na akasema: Imani ni kumuamini Mwenyezi Mungu, yaani: Unamuamini Yeye kuwa ni Mola, Muumba, Mwenye kutoa riziki, Mmiliki, na Mdhibiti wa kila kitu, na unamuamini kuwa ni Mwenyezi Mungu anayeabudiwa na kutiiwa, na unaamini kwamba Yeye ana Majina Mazuri Zaidi na sifa za juu kabisa.

12.  Kuamini Malaika, ni kuamini uwepo wao, na kwamba wameumbwa kutokana na nuru, wala hawamuasi Mwenyezi Mungu juu ya Amri zake, na wanafanya wanayoamrishwa, na kuamini malaika aliowataja Mwenyezi Mungu kwa majina yao. na kazi zao; kama Jibril ni mwenye dhamana ya kufikisha wahyi (ufunuo) na ndiye Malaika mkuu, na Mikaeli amekabidhiwa mvua na mimea, na Israfil amekabidhiwa kupuliza baragumu, na mlinzi wa moto, na kadhalika.

13.  Kuamini vitabu ni: Kuamini kwamba ni wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kwamba ni lazima kuamini yaliyomo ndani yake na kufanyia kazi hukumu zilizothibiti, pia Qur`aan imekuja kufuta sheria zote zilizokuwa kabla yake, kwa kuwa Torati na Injili ni vitabu ambavyo vimepotoshwa na kubadilishwa.

14.  Kuamini Mitume ni: kuamini waliyoyaleta, na kwamba Mwenyezi Mungu amewateremshia amri yake, na kwamba wao ni bora katika viumbe wa Mwenyezi Mungu, tunawaamini wote, waliotajwa katika Qur-aan na Sunnah na sisi tunaijua hadithi yake, na ambaye hatujui chochote juu yake, na wala hatutofautishi baina ya yeyote kati yao. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

“Hakika wale wanao mkataa Mwenyezi Mungu na Mitume wake, na wanataka kufarikisha baina ya Mwenyezi Mungu na Mitume wake, kwa kusema: Wengine tunawaamini na wengine tunawakataa. Na wanataka kushika njia iliyo kati kati ya haya (50) Hao ndio makafiri kweli kweli. Na tumewaandalia makafiri adhabu ya kudhalilisha (51) Na walio muamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake, wala wasimfarikishe yeyote kati yao, hao atawapa ujira wao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira, na Mwenye kurehemu”.

[An-Nisa: 150-152].

15.  Kuamini Siku ya Mwisho ni: Kuamini kufufuliwa na kuhesabiwa, na kuamini uwepo wa Pepo na moto, na Njia na Mizani, na Uombezi wa Mtume na Mto wa Al-Kawthar, na mambo mengine yote ambayo habari zake Zimethibitishwa Katika qur`ani na Sunnah.

16.  Kuamini makadirio ni: kuamini kwamba Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu na utukufu, anayajua matendo ya waja na yatakayowapata, na kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu aliandika yote katika Ubao Uliohifadhiwa kabla ya kuumbwa viumbe, na kwamba matendo ya waja hufanyika kwa mujibu wa yale yalioandikwa katika elimu na maandishi ya Mwenyezi Mungu, na kwamba matendo ya waja wote yameumbwa na Mwenyezi Mungu. Kama vile kukanusha na kuamini, kutii na kuasi.[2]

17.  Kisha akamuuliza kuhusu Ihsani ambayo ni daraja la tatu la dini, akamwambia kuwa Ihsani ni mtu kuMuabudu  Mola wake kwa ukamilifu kabisa kana kwamba anamuona mbele yake. Ikiwa mtu hakufikia kiwango hicho cha kuhisi kumuona Mwenyezi Mungu na kuogopa, basi ahisi kuwa Mwenyezi Mungu, anamuona. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

“Na mtegemee Aliyetukuka Mwenye nguvu, Mwingi wa Rehema (217) ambaye anakuona unapoinuka (218) na kugeuka kwako kwa kusujudu (219) kwa hakika yeye ni mjuzi na msikivu Zaidi. (219).

[Al-SShuaraa: 217 - 220]

Daraja za dini zote zimefungamana kwani; Uislamu ni wa neno la jumla zaidi kuliko imani na ihsan, na vyote viwili vimejumuishwa humo, imani imejumuisha zaidi kuliko Ihsani, kwa hivyo anayetoka katika daraja la imani bado ni Mwislamu, na anayetoka katika daraja la ihsani bado yuko kwenye cheo cha imani. Amesema Mwenyezi Mungu:

“Mabedui walisema: “Tumeamini.” Sema: “Hamjaamini.” Lakini semeni: “Tumesilimu.” Na Imani bado haijaingia katika nyoyo zenu”.

[Al- hujraat: 14]

18.  Kisha muulizaji akamuuliza kuhusu kiyama, Kitasimama lini? Yeye, (Rehma na amani ziwe juu yake), alisema: “Mwenye kuulizwa sio mjuzi zaidi kuliko muulizaji.” Yaani elimu yangu juu yake si zaidi ya yako. Hakuna ajuaye wakati wake isipokuwa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu amesema

“Mwenyezi Mungu ana ujuzi wa kiyama”

[Luqman: 34].

19.  Basi akabadilisha swali hili kwa kumuuliza juu ya ishara zake, basi Mtume akamjibu kwamba moja ya ishara zake ni kwamba kijakazi atakapomzaa bosi wake, ambayo ina maana ya kwamba watumwa kuwa wengi mpaka kufikia kijakazi kumzaa binti wa bosi, hivyo huyo binti atakuwa ni mtu huru, hali ya kuwa mama ni kijakazi. Au kwa maana nyingine ni wajakazi kuzaa wafalme, Au: Wasiokuwa Waarabu kuzaa Waarabu, na Waarabu ni mabwana na watukufu wa watu.[3]

20.  Alama zake nyengine ni kuwa masikini waliokuwa wakitembea peku na bila viatu, nakuwa uchi na hawapati kitu cha kusitiri katika mavazi, wachungaji na mabedui, wanakuwa matajiri na wenye mali, na kuanza kushindana katika kujinga majumba ya kifahari. Na Pengine hii inarejea kwenye Hadith inayosema: “Iwapo jambo atapewa asiyestahili, basi ingoje kiyama”[4], kama mambo wanapewa wale wasiostahiki, mpaka wakawa mabedui na wajinga ndio viongozi wa watu, wakawa kati ya wanaomiliki mali na ufahari.[5]

21.  Kisha yule mtu akaondoka, na Umar akakaa kwa muda mfupi, kisha Mtume, amani iwe juu yake, akamwambia: Je, umemjua mtu huyu ni nani? Umar akasema: “Mwenyezi Mungu na Mtume wake ndio wanajua zaidi.” Akasema (Rehma na amani ziwe juu yake): Huyu ni Jibril, amekuja kukufundisha dini yenu.

Mwenyezi Mungu Mtukufu amewapa Malaika uwezo wa kuchukua sura ya wanadamu viumbe wengineo, na Jibril, amani iwe juu yake, alikuwa akimjia Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, mara kwa mara katika sura ya Dahiya al-kalbiyyu swahaba wa mtume amani iwe juu yake. 

Mafunzo

  1. Jibril, amani iwe juu yake, alipoingia kwa Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake) alikaa mkao wa mwenye kutafuta elimu akiwa makini na tayari kukubali elimu anayopewa, bila ya kuwa na kiburi licha ya utukufu wake. naye ndiye mwenye dhamana ya kufikisha ufunuo na ni Roho Mtakatifu. Hapo tunajifunza kuwa na adabu na ni kwa kila anaemuuliza mwanachuoni azingatie adabu hiyo katika kukaa naye, na wala asimuulize kwa sura ya mtu mwenye kiburi, mwenye kujitosheleza, kama vile kukaa kwa kuegemea, au kutoa sauti isiyofaa.

  2. Nguzo za Uislamu ni miongoni mwa mambo ya mwanzo ambayo Muislamu anatakiwa kuyasimamia katika mipango yake ya kila siku na kila mwaka, kujilazimisha kuzifuata, na kukamilisha kila moja katika utendaji wake: basi atazame nguvu ya kukiri kwake kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kuukamilisha kwa kumtaja sana Mwenyezi Mungu, na kuboresha Swala yake. Na azidishe kusali sala za sunnah, kama vile ibada zisizo za wajibu, na Sunna za kawaida, na mawaidha ya swalah, na kutoa zaka kamili kwa wema, na kutoa sadaka mbalimbali, pia kufunga Ramadhani na asiiharibu kwa kufanya madhambi, aongeze utiifu kwa kujitolea. Na Kuhiji Nyumba ya Mwenyezi Mungu hata mara moja, na kuongeza anachoweza, kama Hajj na Umra.

  3. Jitahidi kutekeleza kila nguzo ya imani, na jiulize moyo wako ulifanya nini katika kila nguzo hizo, na vipi imani yako kwa Mwenyezi Mungu juu ya kustahili kuabudiwa kwake, na uungu wake, majina na sifa zake? ni ipi thamani ya Malaika na heshima yao kwako? Na Unafuraha kiasi gani juu ya vitabu vya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa viumbe vyake, na kuvitukuza, hasa hasa Qur’an? Je! Kiasi gani unawaheshimu Mitume wake, na mapenzi yako kwao je, ni mapenzi yanayokuiteni kuuliza undani wa maisha yao, ni ipi thamani yenu kwa Siku ya Mwisho na je, mnaikumbuka daima? Je! ni kiasi gani unaamini makadirio Ya Mwenyezi Mungu? Na kuridhika na yote yanakukuta?

  4. Kiwango cha juu kabisa cha Dini ni daraja ya Ihsani, je umejaribu kujilazimisha kumuabudu Mungu kana kwamba unamuona, au usipomuona basi kumbuka kuMuabudu  Mwenyezi Mungu, na jua kwamba Yeye anakuona vizuri kuliko ungewezeshwa kumuona. Mwenyezi mungu si rahisi kuonekana kwako.

  5. Ikiwa mtu ana hakika na anahisi uwepo wa Mwenyezi Mungu, kuonekana kwake mbele ya Mwenyezi Mungu na uchunguzi wake juu Yake, basi angeona aibu MwenyeziMungu kumuona mvivu katika kumtii, achilia mbali kumuona akifanya uasi. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

    “Na mtegemee Aliyetukuka Mwenye nguvu, Mwingi wa Rehema (217) ambaye anakuona unapoinuka (218) na kugeuka kwako kwa kusujudu (219) hakika yeye ni mjuzi na msikivu.

    [As-Shuaraa:217-220]

  6. Uislamu umeitukuza siku ya mwisho, japo haukubainisha wakati wake, lakini ikajulishwa dalili zake, nazo na nyenginezo zinatuhimiza kuikumbuka siku hiyo mara kwa mara, je ni lini tulikaa kuifikiria siku ambayo haiepukiki? 

Marejeo

  1. tazama “Sharh Riyadh as-Salihin” cha Ibn Uthaymiyn (1/347).
  2. “Jami’ al-Ulum wa al-Hakam” cha Ibn Rajab (1/103).
  3. Tazama: “Jami’ al-Ulum wa al-Hakam” cha Ibn Rajab (1/136-137).
  4. Imepokewa Na Al-Bukhari, Na.: (59), Kwa Kutoka Kwa Abu Hurairah
  5. Tazama: “Jami’ al-Ulum wa al-Hakam” cha Ibn Rajab (1/139).

Miradi ya Hadithi