عن أبي هريرةرضي الله عنه أن رسول الله ﷺ قال: «أَحَبُّ الْبِلَادِ إِلَى اللهِ مَسَاجِدُهَا،وَأَبْغَضُ الْبِلَادِ إِلَى اللهِ أَسْوَاقُهَا»
عن أبي هريرةرضي الله عنه أن رسول الله ﷺ قال: «أَحَبُّ الْبِلَادِ إِلَى اللهِ مَسَاجِدُهَا،وَأَبْغَضُ الْبِلَادِ إِلَى اللهِ أَسْوَاقُهَا»
Kutoka kwa Abu Hurayrah Mwenyezi Mungu awe radhi naye kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu rehma na Amani zimshukie amesema:
“Nyumba zinazopendwa zaidi na Mwenyezi Mungu ni misikiti yake. Maeneo yanayochukiwa zaidi na Mwenyezi Mungu ni Masoko ’’.
Amesema Mtume Rehema na Amani zimshukie kuwa misikiti ni sehemu zinazopendwa zaidi na Mwenyezi Mungu. Ni nyumba ya utiifu, msingi wa uchamungu, sehemu za kumtaja mola mlezi, vyanzo vya elimu, na mahali pa kupatikana wito wa Mwenyezi Mungu.
Ndio maana Mtume Rehema na Amani zimshukie alikuwa na shauku ya kuujenga msikiti alipofika Madina mara ya kwanza, na alikuwa akibeba mawe yeye mwenyewe, amani iwe juu yake, pamoja na maswahaba zake, Mungu awe radhi nao.
Msikiti ni jengo la kwanza katika kuunda dola ya Uislamu, na kutoka humo huenezwa daawah, na ndani yake hufunzwa hukumu na sheria za Kiislamu, na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kupitia msikiti aliweza kusimamia mambo ya dola, na ndani ya msikiti aliweza kujadiliana na Maswahaba mipango ya vita na uvamizi, kupokea misafara na wajumbe, wa makampuni ya kutekeleza, kuwasuluhisha wagomvi na kadhalika.
Wanaokwenda Misikitini ni watu wa Imani na khofu, ambao Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema juu yao:
“Katika Nyumba ambazo Mwenyezi Mungu ameamrisha zitukuzwe, na humo litajwe jina lake, wanamtakasa humo asubuhi na jioni (36) Watu ambao biashara wala kuuza hakuwashughulishi na kumdhukuru Mwenyezi Mungu, na kushika Sala, na kutoa Zaka. Wanaikhofu Siku ambayo nyoyo na macho yatageuka”
[An-Nur: 36-37].
Aliwataja kuwa na imani kwa kusema:
“Hakika wanao imarisha misikiti ya Mwenyezi Mungu ni wale wanao muamini Mwenyezi Mungu, na Siku ya Mwisho, na wakashika Sala, na wakatoa Zaka, na wala hawamchi ila Mwenyezi Mungu. Basi huenda hao wakawa katika waongofu”
[At-Tawbah: 18].
Kwa hiyo kujitolea katika kujenga nyumba za Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiko kujitolea kwa hali ya juu zaidi, Mtume Rehma na Amani ziwe juu yake amesema: “Mwenye kujenga msikiti kwa kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu atamjengea mfano wake peponi[1]”
2. Na Mtume Rehema na Amani zimshukie ametuambia kuwa sehemu zinazochukiwa zaidi duniani ni masoko. Pale ambapo kuna utata, mazungumzo ya kipuuzi, ulaghai, udanganyifu, viapo vya uwongo, miamala ya riba, kuvunja ahadi, kupuuza kumkumbuka Mwenyezi Mungu, na kadhalika. Ndio maana Salman al-Farsi Mwenyezi Mungu awe radhi naye akasema kwamba masoko ni “vita vya Shetani; na huweka bendera yake masokoni[2]”
Ameeleza Mtume kuwa misikiti ni sehemu zinazopendwa zaidi na Mwenyezi Mungu, na hii inapelekea kuwa kufanya ibada ndani yake ni bora kuliko kufanya ibada sehemu nyengine; Kuswali msikitini ni bora kuliko kuswali nyumbani na sokoni, na mikusanyiko ya elimu msikitini ni bora kuliko sehemu nyingine yoyote, na kujitolea kujenga misikiti ni bora na kuna thawabu zaidi kuliko kutoa sadaka katika njia zingine.
Kukua kwa Uislamu na siri ya maendeleo yake ilikuwa katika kuitumia nafasi na umuhimu wa msikiti kimalezi, kiulinganiaji na kielimu. Ikiwa tunataka kurejea kwenye njia ya ustaarabu, ni lazima tuchunge malezi sahihi na kuitambua nafasi ya msikiti katika Nyanja hiyo.
Iwapo msikiti ni sehemu inayopendwa zaidi na Mwenyezi Mungu Mtukufu, basi hapana shaka kuwa kukaa humo kwa nia ya ibada na kungojea Swala kuna malipo makubwa, na Muislamu hatakiwi kuukosa kiasi hicho cha malipo kwa namana awezavyo.
Mwenyezi Mungu, aliyetakasika, amefanya kwenda Misikitini kuwa miongoni mwa matendo makubwa yanayomkurubisha mja kwa Mola wake Mlezi, Aliyetukuka, Mtukufu. Hata Mtume, amani iwe juu yake, ameeleza katika wale saba ambao Mwenyezi Mungu atawatia chini ya kivuli chake siku ambayo hakutakuwa na kivuli isipokuwa chake: "Na mtu ambaye moyo wake umeshikamana na misikiti[3]"
Misikiti ni nyumba za Mwenyezi Mungu.imewekewa adabu ambazo Muislamu anatakiwa kuzizingatia; ikiwa ni pamoja na Kuvaa nguo nzuri, na kujipamba, na kujipaka manukato kwa yale aliyo nayo, na kuacha vyakula vyenye harufu mbaya, kama vile kitunguu saumu, na mengineyo, ambayo yanawaudhi Malaika na wana Adam.
Inapendeza kwa Muislamu kuanza kuingia kwake msikitini kwa dua zilizopokelewa katika hadith; Mtume Rehma na Amani ziwe juu yake amesema: “Akiingia mmoja wenu msikitini, na aseme: Ewe Mola nifungulie milango ya rehema yako, na atakapotoka aseme: Ewe Mwenyezi Mungu, nakuomba kwa fadhila Zako.[4]”
Ni Sunnah kwa mwenye kuingia msikitini asikae mpaka aswali rakaa mbili za kusalimia msikiti; Amesema Mtume Rehma na Amani ziwe juu yake: “Mmoja wenu anapoingia msikitini basi asikae mpaka asali rakaa mbili[5]”
Masoko ni sehemu mbaya zaidi kwa sababu ya madhambi, uchafu, mabishano na mambo mengine yaliyomo ndani yake, na sehemu yoyote inayofanana na hiyo katika matatizo basi itachukua hukumu hiyo. Ikiwa nyumba na mahali pa kazi ya mtu hupatikana viapo vya uwongo, uasherati, kutukana, na kadhalilika; Itakuwa ni moja ya sehemu mbaya sana mbele ya Mwenyezi Mungu.
Haipendezi kwa mtu kwenda sokoni bila ya haja, lakini akienda kwa ajili ya haja kama vile kununua na kuuza haichukiwi; Hakika Yeye Aliyetukuka anasema:
“Na hatukuwatuma kabla yako Mitume ila walikula na kwenda masokoni ’’
[Al-Fuqan: 20].
Mwenye kuchochewa na haja ya kwenda sokoni asiwe wa kwanza kuingia humo, wala asiwe wa mwisho kutoka humo; Kama Salman al-Farsi Mwenyezi Mungu awe radhi naye alivyosema: “Usiwe - ukiweza - wa kwanza kuingia sokoni, wala wa mwisho kutoka humo; Ni vita vya Shetani, na hunyanyua bendera yake[6]”
Mshairi alisema:Yeyote anayeshikamanisha moyo na msikiti na haMuabudu yeyote isipokuwa mkarimu, mwenye kuneemesha Basi huyo ndiye atakuwa chini ya kivuli cha Mwenyezi Mungu wakati ambao= Hakuna kivuli ila chakwake, Aliyetakasika milele Mwenye kuogopa madhambi huja akitetemeka = na hakimbilii popote ila msikitini nyumba imara.
Basi akamtukuza Mwenyezi Mungu, akaomba, kwa unyenyekevu = katika nyumba ambayo haabudiwi kwa haki isipokuwa yeye. Inapokuwa safi roho na nafsi yake, = basi hawezi kuwa na dhulma, wala husuda moyoni.Na ni waovu wangapi walikuwa wakija huku wamezama katika maasi = akarejea alibeba mbavuni mwongozo Na ni wajinga wangapi, wamegubikwa na giza la ujunga = ukawa mwezi kamili wenye nuru ya elimu iwakayo.