عن ابن عبَّاسٍ رضي الله عنهما قال: كنتُ خَلْفَ رسولِ الله ﷺ يومًا، فقال: «يا غلامُ، إنِّي أُعلِّمُكَ كلماتٍ: احْفَظِ اللهَ يَحْفَظْكَ،احفَظِ اللهَ تَجِدْه تُجاهَكَ،إذا سألْتَ فاسأَلِ اللهَ، وإذا استَعَنْتَ فاستَعِنْ باللهِ، واعلَمْ أنَّ الأُمَّةَ لوِ اجتَمَعَتْ على أنْ يَنفَعوكَ بشيءٍ، لم يَنفَعوكَ إلَّا بشيءٍ قد كتَبَه اللهُ لكَ، ولوِ اجْتَمَعوا على أنْ يَضُرُّوكَ بشيءٍ، لم يَضُرُّوكَ إلَّا بشيءٍ قد كتَبَه اللهُ عليكَ، رُفِعَتِ الأقلامُ وجَفَّتِ الصُّحُفُ»

Kutoka kwa Ibn wa Abbaas (Radhi za Mwenyezi ziwe juu yake), amesema: Siku moja nilikuwa nyuma ya Mtume wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, akasema:

1. “Ewe kijana, hakika mimi ninakufundisha maneno (haya): 2. Mhifadhi Mwenyezi Mungu 3. Ili naye akuhifadhi 4. Muhifadhi Mwenyezi Mungu utampata mbele yako (kwa kila jambo lako) 5. Pindi utakapo omba, muombe Mwenyezi Mungu 6. Na ukitaka msaada basi taka msaada  kwa Mwenyezi Mungu 7. Tambua kwamba jamii ikikubaliana kukusaidia kwa lolote, haiwezi kukusaidia ila jambo ambalo Mwenyezi Mungu amekuandikia, na lau ikikubaliana ikudhuru kwa lolote, haiwezi kukudhuru ila kwa jambo ambalo Mwenyezi Mungu amekuandikia. 8. Kalamu imesha nyanyuliwa na karatasi zimesha kauka.  

Ibn Abbaas (Radhi za Mwenyezi ziwe juu yake) alikuwa nyuma ya Mtume (Rehma na Amani ziwe juu yake) wamepanda mnyama.

1.Mtume (Rehma na Amani ziwe juu yake) akataka amfundishe somo linalo husu kumuamini Mwenyezi Mungu Mtukufu. Ili kuvuta usikivu na akili yake, akumuita kulingana na umri wake, alikuwa ni kijana mwenye umri wa miaka kati ya kumi hadi kumi na nne, akamwambia: “hakika mimi ninakufundisha maneno” akimaanisha: uyahifadhi, uyaelewe na uyafanyie kazi.

2. Jambo la kwanza alilo mfundisha ni, amuhifadhi Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa kuto vunja mipaka aliyo iweka na kutekeleza aliyo amrisha, aamrishe aliyo muamrisha Mwenyezi Mungu Mtukufu na akataze aliyo mkataza.

amesema Mwenyezi Mungu:

" Na wanao linda mipaka ya Mwenyezi Mungu ".

 [At-Tawbah: 112]

Amesema Mwenyezi Mungu :

32. "Haya ndiyo mnayo ahidiwa kwa kila mwenye kurejea kwa Mwenyezi Mungu na akajilinda.33. Mwenye kumwogopa Mwingi wa Rehema hali yakuwa hamwoni, na akaja kwa moyo ulio elekea” .

[qaaf: 32, 33]

3. Mwanadamu anapo hifadhi mipaka ya Mola wake na akatekeleza maamrisho yake, atalipwa kwa matendo yake, kama anavyo muhifadhi Mwenyezi Mungu Mtukufu, pia Mwenyezi Mungu Mtukufu anamuhifadhi. Hifadhi ya Mwenyezi Mungu inajumuisha kuhifadhi mwili, viungo, akili na vinginevyo.

Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

“Kila mtu analo kundi la malaika mbele yake na nyuma yake linamlinda kwa amri ya Mwenyezi Mungu.”

[ra`ad: 11]

Hifadhi ya Mwenyezi Mungu haikomei kwa huyu anaye hifadhi mipaka yake tu, bali humuhifadhia familia yake pia, amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na wachelee wale ambao lau kuwa na wao wangeli acha nyuma yao watoto wanyonge wangeli wakhofia. Basi nao wamche Mwenyezi Mungu, na waseme maneno yaliyo sawa.”. Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:“ Na baba yao alikuwa ni mtu mwema.”.

Na daraja la juu la Mola kumuhifadhi mja wake ni kumuhifadhia dini yake, kumuhifdhi dhidi ya wasiwasi na mienendo ya shetani, amesema

Mwenyezi Mungu Mtukufu:

“Hayo hivyo ni kwa ajili tumuepushe na uovu na uchafu. Hakika yeye alikuwa katika waja wetu walio safishwa..

 [Yusuf: 24]

  Na ndio maana amesema Ibn Abbaas akitafasiri 

Mwenywzi Mungu Mtukufu:

“Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu huingia kati ya mtu na moyo wake, na kwamba hakika kwake Yeye tu mtakusanywa.”

[Al-Anfal: 24]

 Anamkinga muumini dhidi ya maasi ambayo yatampeleka Motoni.[1]

4. Kisha Mtume (Rehma na Amani ziwe juu yake) akataja malipo mengine ya anaye hifadhi mipaka ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, nayo ni Mwenyezi Mungu kuwa naye Maisha yake yote, anamsaidia, anamlinda, anampa nguvu, anamjibu maombi yake na anakubali ibada zake; amesema Mtume Mtukufu, amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na mja anapo endelea kujiweka karibu na mimi kwa kutekeleza ibada za Sunna, (za hiyari) mpaka ninampenda, nikimpenda, ninakuwa sikio lake analotumia kusikia, na jicho lake analotumia kuona, na mkono wake anaotumia kushika, na mguu wake anaotumia kutembea, na akiniomba kwa hakika ninamjibu, na akinitaka ulinzi kwa hakika ninamkinga " [2]

5. ,Kisha Mtume Mtukufu akamuelekeza mlango Mtukufu katika milango ya Tawhiid na itikadi sahihi, nao ni kumuabudu Mwenyezi Mungu Mtukufu peke yake, na katika maombi asimuombe yeyote zaidi yake, kwa sababu dua ni ibada, haitakiwi kuielekeza kwa asiye kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, amesema Mtume S.A.W: “Dua ni ibada”

kisha akasoma:

“Na Mola wenu Mlezi anasema: Niombeni nitakuitikieni. Kwa hakika wale ambao wanajivuna na kuniabudu Mimi wataingia katika Jahannamu hali ya kudhalilika.”

[Ghafir: 60]

[3], kwa sababu katika dua kuna kudhihirisha udhalili na uhitaji wa muombaji, lakini pia kukili kwamba anaye ombwa ana uwezo wa kuleta manufaa na kuzuia madhara, na haifai kujidhalilisha ila kwa Mwenyezi Mungu pekee; kwa sababu hiyo ndio ibada ya kweli.[4]

6. Kisha Mtume (Rehma na Amani ziwe juu yake) akamuamrisha awe anamuomba msaada Mwenyezi Mungu Mtukufu pekee. Kuomba masaada; ni uhitaji wa msaada ili kufikia malengo. Kuomba msaada ni kudhihirisha jinsi unavyo mtegemea Mwenyezi Mungu Mtukufu. Tawhiid katika kuomba msaada tumejifunza katika kauli ya

Mwenyezi Mungu Mtukufu:

“Wewe tu tunakuabudu, na wewe tu tunakuomba msaada "

[Al-Fatihah: 5]

. kwa sababu alipo waamrisha waja wake wamtii, aliwaelekeza wamuombe yeye pekee, na wamuombe awaongoze waache maasi na wafanye ibada.[5]

Ieleweke kwamba, kumuomba msaada kiumbe katika jambo analoliweza inaruhusiwa. Mwanadamu anaweza kumuomba mwanadamu mwenzake amsaidie kubeba mzigo au amsaidie jambo ambalo kwa kawaida mwanadamu analiweza. Inapendeza kwa mwislaam kusaidia jambo ambalo analiweza, Mtume (Rehma na Amani ziwe juu yake) amesema: “Na ukimsaidia mtu, kwa kumbeba juu ya mnyama wake, au kumsaidi kupakia mzigo wake ni sadaka”[6]. Kuomba msaada ambako ni haramu, ni katika vitu ambavyo haviko katika uwezo wa anaye ombwa, bali anaviweza Mwenyezi Mungu pekee, kama kuwaomba maiti, kuomba kwa kupitia makaburi ili upone maradhi au ufaulu mtihani au upate mtoto, kufanya hivyo ni haramu.

7 .Kisha Mtume (Rehma na Amani ziwe juu yake) akamfundisha Ibn Abbaas kusalenda, kuridhia mipango ya Mwenyezi Mungu na kumtegemea kiukweli, kwa sababu mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na yote yanayo msibu mja, mabaya au mazuri yanatoka kwake, ameandika yampate kabla hajaumba mbingu na Ardhi. Hata kama viumbe wakikubaliana kuzuia aliloliandika limpate, hawawezi kufanikisha, na hata wakikubaliana kumnufaisha au kumdhuru kwa jambo ambalo hajaliandika, mipango yao haiwezi kufaulu hata kidogo. Amesema

Mwenyezi Mungu Mtukufu:

“Na Mwenyezi Mungu akikugusisha madhara, basi hapana wa kukuondolea ila Yeye. Na akikutakia kheri, basi hapana awezaye kurudisha fadhila yake" 

[Yunus: 107]

”. Ibara hii ndio imebeba ujumbe wa usia huu, kwa sababu mja anapo tambua kwamba halimpati lolote ila alilo liandika Mwenyezi Mungu, na kwamba juhudi za viumbe hazina nafasi, hilo linamfanya amtegemee Mwenyezi Mungu Mtukufu kiukweli, ajisalimishe mbele yake, atekeleze maamrisho yake na kuacha makatazo, aidha kuipa kauli yake kipaumbele zaidi kuliko kauli yoyote, na haogopi wala hamuombi yeyote zaidi yake.[7]

8.Kisha Mtume (Rehma na Amani ziwe juu yake) akaeleza kwamba kalamu zilizo andika mambo yote yatakayo wapata viumbe zimezuiliwa kuandika, na vitabu vilivyo andikwa yamethibitishwa yote yaliyo andikwa, hakuna marekebisho.

Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

" Hautokei msiba katika ardhi wala katika nafsi zenu ila umekwisha andikwa katika Kitabu kabla hatujauumba. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi”.

[Al-Hadid: 22]

. Na “Mwenyezi Mungu Mtukufu ameandika mambo yote yatakayo wapata viumbe miaka hamsini elfu kabla hajaumba mbingu na Ardhi”[8]

MAFUNDISHO

1.Mtume (Rehma na Amani ziwe juu yake) alikuwa anatumia muda wake na wa maswahaba zake kwa kumtii Mwenyezi Mungu, hata wakiwa wamepanda mnyama..

2.Shauku ya Mtume (Rehma na Amani ziwe juu yake) ya kumfundisha Ibn Abbaas japo ni mdogo kiumri, hadith yenye maana pana katika upande wa mwenendo, tawhiid na mambo yanayo tusibu na mengine mengi, hii inatufundisha kwamba haifai kuwapuuza watoto, hasa waelevu, lakini pia kila mmoja afikishiwe kwa lugha inayo endana naye, hasa katika kufundisha mambo muhimu katika dini, kwani hao ndio vijana wa kesho na ndio nguzo ya jamii kutengemaa 

3.Mtume (Rehma na Amani ziwe juu yake) ameanza mazungumzo yake kwa kumuita na kumvuta msikilizaji, ni maneno machache nayenye maana pana, jambo ambalo linamfanya mtu kuwa makini na hili ni jambo ambalo linatakiwa kwa kila mwenye kutoa nasaha alizingatie. Afungue nasaha zake kwa jambo lenye kumfanya mpokeaji kuzitamani nasaha zake.

4.Mtume (Rehma na Amani ziwe juu yake) hakurefusha usia wake, bali yalikuwa ni maneno machache, hilo linapelekea kufahamika na kufanyiwa kazi, hasa kwa watoto.

5.Kama kweli unajipenda, basi muhifadhi Mwenyezi Mungu Mtukufu ili naye akuhifadhi, wamesema baadhi ya wema walio tangulia: “Mwenye kumcha Mwenyezi Mungu, amejihifadhi mwenyewe, asiye mcha amejipoteza mwenyewe na Mwenyezi Mungu hana shida naye”[9]. Hata kama unahitaji kuhifadhi afya yako, basi muhifadhi Mwenyezi Mungu Mtukufu, kuna mwanazuoni alifikisha zaidi ya miaka mia moja lakini bado alikuwa na neema ya nguvu na akili, siku moja katika matembezi akakutana na mtaro akauruka kwa nguvu, wanafunzi wake wakashangazwa sana, kwa umri wake na jinsi alivyo ruka, akasema: viungo hivi tumevihifadhi dhidi ya maasi tukiwa wadogo, Mwenyezi Mungu akavihifadhi tulipo kuwa wakubwa[10].

6.Imepokelewa kwamba kuna mwanamke alitoka kuelekea vitani pamoja na waislaam, akaacha mbuzi kumi na mbili na kifaa alicho kuwa akikitumia kushona, alipo rudi hakukuta mbuzi wala kifaa chake cha kushonea, akasema: Eh Mola wangu, hakika umechukua dhamana ya kumuhifadhia yeyote anaetoka kwa ajili ya Dini yako, na mimi nimepoteza mbuzi wangu na kifaa changu cha kushonea, nakuomba Mola wangu unirejeshee mbuzi na kifaa change”, alikuwa akimuomba Mola wake mara kwa mara, alipo amka akakuta mara mbili ya mbuzi zake na vifa viwili”[11]

7.Mja anapotaka hifadhi yake, ya familia na mali zake, basi amche Mwenyezi Mungu Mtukufu, amesema Ibnul Munkadir -Mwenyezi Mungu amrehemu-: “Hakika Mwenyezi mungu humuhifadhia mtu mwema mwanae, mjukuu wake na nyumba zinazo mzunguka, wanakuwa katika himaya na sitara yake”[12]. Na Said bin Musayyib -Mwenyezi Mungu amrehemu- alimwambia mwanae: (mimi ninairefusha sala yangu kwa matarajio ya kukuhifadhi, akasoma maneno ya Mwenyezi

Mungu Mtukufu yasemayo:

" Na baba yao alikuwa ni mtu mwema."

[kahf: 82] [13]

8.Namna za kuomba na kuabudu viumbe zinaibuka mpya kila kukicha, kama kuomba nguvu za kiulimwengu au wazazi baada ya kifo. Mfano wa hayo ni filam, vinyago vya kuchezea watoto na semina zenye kujihusisha na imani za kipagani.  Kuwa makini, ushirikina unaibuka ukiwa na majina tofauti.

9.Jiepushe na ibada ya kuomba viumbe hata kama ni kidogo, na ujizoeshe kujihudumia mwenyewe, Mtume (Rehma na Amani ziwe juu yake) alichukua ahadi ya kiapo kwa baadhi watu juu ya mambo kadhaa, miongoni mwa mambo hayo ni: “ Na wala msiwaombe watu chochote”, mpokeaji wa hadith hii amesema: nilimuona mmoja wao, fimbo yake inadondoka akiwa juu ya mnyama, na wala hamuombi yeyote amuokotee[14], jambo hili hata kama si haramu, lakini ni msukumo wa tabia njema na kujitunzia heshima kwa kuepuka masimango ya wanadamu, aidha kujifunza tabia ya uvumilivu katika kipindi cha shida, pia kujitunzia heshima na kuto hitaji misaada ya watu. Walipo kula kiapo, walitekeleza hata katika mazingira ambayo si makusudio yake, ili kufunga milango na njia zote zenye kupelekea kukivunja.[15]

10.Omba msaada kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa mambo yenye kukunufaisha katika Dini na Dunia yako, kama kudumisha Sala, kuwa na tabia njema, katika masomo  na kutafuta kazi, hakuna chenye nguvu kuliko kumuomba Mwenyezi Mungu msaada, Mtume Mtukufu amekuuusia: “pupia kufanya lenye kukunufaisha na umuombe Mwenyezi Mungu msaada”[16] kithirisha kumuomba Mwenyezi Mungu msaada, Mtume (Rehma na Amani ziwe juu yake) alimwambia Muadh bin Jabal: “nakuuusia ewe muadh, usiache kusema mwisho wa kila sala: Eh Mwenyezi Mungu nakuomba unisaidie niwe nakutaja, kukushukuru na kukuabudu kwa Ufanisi”[17]

11.Ni kwa kiasi gani tunawategemea viumbe? Na ni kwa kiasi gani tunamtegemea Mwenyezi Mungu Mtukufu?. Wahabu bun Munabbih -Mwenyezi Mungu amrehemu- alimwambi mtu aliye kuwa akienda kwa wafalme: “una nini! Unaenda kwa mtu ambae anafunga mlango wake na kukuacha nje, ana kuonyesha kwamba ni fukara, na anaficha utajiri wake, unamuacha ambae anafungua mlango wake nusu ya usiku na nusu ya mchana, na anakuwekea wazi utajiri wake, anakwambia: niombe, nami nitaitikia maombi yako”[18]

12.Kuwa na shauku ya kujifunza hadith hii, kuifanyia kazi, na kumfundisha mkeo,mwanao na watu wengine, kila mmoja kulingana na lugha, umri na utayari wake, kwa sababu imebeba usia mzito, kiasi cha baadhi ya wanazuoni kusema: nimeisoma kwa mazingatio hadith hii ikanishangaza karibia nipagawe, ni msiba mkubwa kutoijua hadith hii, na kuielewa  kwa juu juu![19]

13.Amesema mshairi: usimuombe mwanadamu akutatulie matatizo***muombe ambae milango yake haifungwi

Mwenyezi Mungu anachukia usipo muomba***na mwanadamu akiombwa anachukia.


 

Marejeo

  1. Tazama: “Jami’ al-Ulum wa al-Hakam” cha Ibn Rajab (1/470).
  2.   Al-Bukhari (6502), kutoka kwa  Abu Hurairah 
  3.   Abu Dawood (1479), al-Tirmidhiy (3247), na al-Nasa’i katika “Al-Sunan al-Kubra” (3828), na al-Tirmidhiy amesema: Ni nzuri na ni sahihi
  4. .  Tazama: “Jami’ al-Ulum wa al-Hakam” cha Ibn Rajab (1/481)
  5. .   Tazama: “nur aliaqtibas fi wsyat alnby, liibn Abbas” cha Ibn Rajab (uk. 93)
  6. .  Al-Bukhari (2989), na Muslim (1009), kutoka kwa  Abu Hurayrah
  7. .  “Jami’ al-Ulum wa al-Hakam” cha Ibn Rajab (1/484).
  8.   Muslim (2653).
  9.   “Nur Aliaqtibas Fi Wsyat Alnby Liabn Ebbas"Kwa Ibn Abbas” cha Ibn Rajab (uk. 54).
  10.   Tazama: “Jami’ al-Ulum wa al-Hakam” cha Ibn Rajab (1/466).
  11.   Ahmad katika “Musnad” yake (34/260), (20664), na al-Haythami aliiweka daraja kuwa ni sahihi katika  “Majma’ al-Zawa’id na Manbi’ al-Fawa’id” (5/277).
  12.   “Jami’ al-Ulum wa al-Hakam” cha Ibn Rajab (1/467).
  13.   “Jami’ al-Ulum wa al-Hakam” cha Ibn Rajab (1/467).
  14. Muslim (1043).
  15.   Al-Mufhim cha Al-Qurtubi (3/86).
  16.   Muslim (1043).
  17.   Abu Daawuud (1522), an-Nasa’i (1303), na an-Nawawii ameiweka daraja ya sahihi katika “Khulas al-Ahkam” (1/468). 
  18.  “Jami’ al-Ulum wa al-Hakam” cha Ibn Rajab (1/481).
  19.  “Jami’ al-Ulum wa al-Hakam” cha Ibn Rajab (1/462).

Miradi ya Hadithi