عَنْ أَبِي مُوسَى الْأَشْعَرِيّ رضى الله عنه، قَالَ: قَامَ فِينَا رَسُولُ اللهِ بِخَمْسِ كَلِمَاتٍ، فَقَالَ: «إِنَّ اللهَ - عزَّ وجلَّ - لَا يَنَامُ،  « وَلَا يَنْبَغِي لَهُ أَنْ يَنَامَ، يَخْفِضُ الْقِسْطَ وَيَرْفَعُهُ، يُرْفَعُ إِلَيْهِ عَمَلُ اللَّيْلِ قَبْلَ عَمَلِ النَّهَارِ، وَعَمَلُ النَّهَارِ قَبْلَ عَمَلِ اللَّيْلِ، حِجَابُهُ النُّورُ - وَفِي رِوَايَةٍ: النَّارُ - لَوْ كَشَفَهُ لَأَحْرَقَتْ سُبُحَاتُ وَجْهِهِ مَا انْتَهَى إِلَيْهِ بَصَرُهُ مِنْ خَلْقِهِ».

Kutoka kwa Abu Musa al-Ash’ariy, (Radhi Za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake) amesema: siku moja Mtume wa Mwenyezi Mungu (Rehma na Amani ziwe juu yake) alisimama na kutueleza mambo matano, akasema:“Hakika Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu na Mtukufu, halali usingizi.Wala hahitajii kulala,Anashusha mizani na kuinyanya.Matendo yote yanayo tendeka usiku hupelekwa kwake kabla ya Matendo ya mchana, na Matendo yote yanayo tendeka mchana hupelekwa kwake kabla ya Matendo ya usiku.Kizuizi (kati yake na viumbe wake) ni Nuru - na katika riwaya: Moto.Akiondoa kizuizi hicho, Utukufu wa uso wake utachoma kila kiumbe ataefikiwa na macho yake katika viumbe wake”

Related by Muslim, 179.


Mtume (Rehma na Amani ziwe juu yake) alisimama mbele ya maswahaba zake, akataja sentensi tano kuhusu Mwenyezi Mungu Mtukufu, nazo ni:

  1. Ya kwanza: kwamba Mwenyezi Mungu Ametakasika Halali Usingizi, kwani usingizi ni upungufu, na Mwenyezi Mungu Mtukufu hana mapungufu yeyote. Bali kila Kiumbe kinahitaji usingizi kwa sababu ya tabu na uchovu, na Mwenyezi Mungu Mtukufu kajitosheleza na hayo, aliumba mbingu Na ardhi bila kupata tabu wala uchovu, Ndio maana Akasema:

    “Mwenyezi Mungu ambaye hapana Mwenyezi mungu anaeabudiwa kwa haki ila Yeye Aliye hai, anayesimamia mambo yote milele. Hashikwi na usingizi wala kulala”

    [Al-Baqarah: 255].

  2.  Ya pili: Mtume (Rehma na Amani ziwe juu yake) alisisitiza sifa hii, kwa kusema: na haiwezekani Mwenyezi Mungu kulala, hivyo sentensi ya kwanza ilimaanisha kutopatikana usingizi kwa Mwenyezi Mungu, na ya pili inamaanisha kuwa haiwezekani kwake kufanya hivyo kamwe [1].

 Bali haiwezekani kwake kulala, kwa sababu usingizi ni uzembe usioendana na ujuzi na usimamizi wa mwenyezi mungu kwa viumbe vyote na itakuwaje asinzie hali ya kuwa ameshikilia mbingu kwa mkono wake. Na ikiwa Mwenyezi Mungu angelala, basi Mbingu zingeanguka chini na mpangilio wa ulimwengu ungevurugika, na hilo haliwezekani kamwe.

3.   ya tatu: Sifa nyengine ni kwamba Mwenyezi Mungu Anasimamia mambo kwa uadilifu, Anaweza kuwapunguzia watu riziki na kuwazidishia wengine, na kuwadhalilisha baadhi ya watu na kuwatukuza wengine, kwa hekima na uadilifu hupima matendo yao kwa uadilifu, huchukua matendo mema na matendo mabaya huyakataa na kuyarudisha, Mola Mtukufu amesema:

“Kwake Yeye hupanda Maneno mazuri na amali njema huinyanyua na kuitukuza”

(Fatir: 10).

4.   Ya nne: Ni kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu, hupelekewa matendo ya waja kila siku, Malaika walio pewa dhamana ya kuandika matendo ya waja wakati wa mchana hupeleka matendo yao kabla ya kuingia usiku, Na wanapeleka matendo ya usiku kabla ya kuingia mchana, bila kuchelewa wala kuchoka.” Amesema Mtume rehma na amani iwe juu yake: “Wanapokezana kwenu Malaika wa usiku na Malaika wa mchana, na wanaakutana nyakati mbili: wakati wa swala ya alfaji na sala ya al-asri, kisha wanaondoka malaika waliokuwa wakiandika matendo yenu. na mola wenu mlezi anawauliza hali akijua kila kitu: vipi mmewaacha waja wangu? Nao wanajibu kwa kusema: tuliwakuta wakiwa wanaswali, na tumewaacha wakiwa wanasali” [2].

5.   Ya tano: kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu kafichikana kutokana na viumbe wake kwa kizuizi cha nuru, na katika riwaya: cha moto; Kwani Yeye Mwenyezi Mungu Anasema:

“Macho hayana uwezo wa kumuona Mwenyezi Mungu bali Yeye anaona viumbe wake, Naye ni Mpole, Mwenye khabari”

[Al-An’am: 103].

Hakuna mgongano kati ya riwaya hizi mbili za nuru na moto. Kwa sababu moto una sifa mbili: kung'aa na kuunguza. Inawezekana Mwenyezi Mungu Mtukufu ameiondosha sifa ya kuungua na akabakisha sifa ya kung'aa, tofauti na moto wa Jahannam. Kwani huo ni moto unaowaka na kuunguza wala hakuna mwanga ndani yake, na nuru hiyo ni tofauti na nuru nyingine zote za dunia kama vile jua na taa; kwani yenyewe imekusanya kung’aa na kuunguza”.[3]

6.   Lau Mwenyezi Mungu angeliondoa pazia hilo, uzuri wake, na fahari yake na mwangaza wake ungeteketeza kila kitu anachokiona na kila chenye kumuona Mwenyezi Mungu, na hatimaye kuungua viumbe vyote; Kwani katika kisa cha nabii Mussa alipomuomba amuone Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu alikataa ila ili kumridhisha mja wake akataka kujidhihirisha katika mlima, mlima huo haukuweza kustahimili hilo pamoja na kuwa nikitu kigumu. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

“Alipo jionyesha Mola Mlezi wake katika mlima, aliufanya uvurugike na kuporomoka.”

[Al-A’raf. 143]

. Hivyo basi Kutakuwa na hali gani endapo atakapo jidhihirisha kwa mwanadamu?

Mafunzo

  1. Jambo kubwa zaidi walilofanya wanazuoni wabobezi katika elimu ya Tauhid (kumpwekesha Mwenyezi Mungu): Ni kuzungumza kuhusu habari za Mwenyezi Mungu, hivyo basi mazungumzo yako yawe mazuri kwa kumtaja Mwenyezi Mungu. Wakati mwingine kuyataja na kwa kueleza kuhusu Majina na Sifa Zake kwa usahihi, na mara nyingine kuhusu maamrisho na makatazo Yake, na mara nyingine kuhusu mawaidha Yake na simulizi za watu wa kale alizosimulia, na mwisho wao ulikuwa vipi na uchukue mazingatio.

  2. Sifa za Mwenyezi Mungu Mtukufu ni katika mambo ya siri, hivyo basi chukua katika maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na Mtume wake, (Rehma na Amani ziwe juu yake), na uyafanyie kazi yale yaliyothibiti, hata yakiwa machache katika mtazamo wako. na uyaamini bila ya kupotosha maana yake, na pasina kumfananisha sifa za Mwenyezi Mungu na sifa za viumbe wake, kwani yeye amesema:  

    “Hakuna anayefanana Naye na Yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona

    [Al-Shura: 11].

  3. Unapotaka kulala elekeza mambo yako yote kwa Mwenyezi Mungu kisha ulale kwa amani kwani Mwenyezi Mungu halali wala hafai kwake kulala, na Mwenyezi Mungu ndiye mlinzi bora, na ni mwingi wa huruma kuliko wenye huruma. Ndio maana tunasema katika Dua kabla ya kulala: “Ewe Mola wangu, nausalimisha uso wangu Kwako, na ninakukabidhi mambo yangu, na nimerejea kwako kwa upendo na khofu, hakuna kimbilio au uokovu isipokuwa kwako tu” [4].

  4. Siku zote kumbuka ukaribu wa Mwenyezi Mungu kwako na kuwa yeye anaona na kushuhudia kila unachofanya, kwani Mwenyezi Mungu halali wakati jicho la dhalimu linapolala, na wala halali wakati mlinzi anapolala ikawa sababu ya kutokea uharibifu kwa sababu ya kulala kwake, na Mwenyezi Mungu halali wakati anapoona ukisimama na kusujudu, ukimwomba akurehemu na aitikie maombi yako.

  5. Ridhika na hukumu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu katika yale anayoyapanga, iwe kakupandisha daraja au kakushusha, kuongezeka riziki au kupungua, utukufu au unyonge, iwe katika masomo, pesa, sifa kutoka kwa watu au wadhifa. Kwani Yeye Mwenyezi Mungu humgawia kila mtu kiasi chake na sehemu yake kwa hekima na uadilifu, hivyo basi kuwa ni mwenye kufanya yanayompendeza Mwenyezi Mungu Mtukufu.

  6. Ni wajibu kwa mja afanye haraka kutubia, na kuomba msamaha kwa makosa aliyoyafanya kabla matendo hayajachukuliwa kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu, “hupelekwa kwake matendo ya usiku kabla ya kuanza kuandika matendo ya mchana, na matendo ya mchana kabla ya kuanza kuandika matendo ya usiku.”

  7. Kimbilia kufanya matendo mema kila usiku na mchana. Dawud al-Twaa’iy – Mwenyezi Mungu amrehemu – amesema: “Usiku na mchana ni vituo ambavyo watu huteremka mmoja baada ya mwingine mpaka mwisho wa safari yao, ukiweza kuandaa akiba itakayokupitisha kila kituo basi fanya hivyo, safari ya Maisha iko ukingoni, na safari hiyo iko haraka Zaidi. jiandae vyema kwa safari yako, na kamilisha yale unayoweza kuyafanya katika kheri, kwani ni kifo kinakuchukua ghafla. [5]

  8. Nafsi zimeumbwa kupenda vizuri katika kila kitu, na hakuna zuri zaidi kuliko Mwenyezi Mungu, na pazia lake ni Nuru, hivyo shikamana na Nuru hiyo.

  9. Jisalimishe kwa Mwenyezi Mungu katika khabari na hukumu zake, kuna mambo ambayo hatujui sababu yake, lakini Mwenyezi Mungu Mtukufu ameyahukumu yatokee kwa hekima na busara zake, kuna mtu anaweza kuuliza: Kwa nini hatumuoni Mwenyezi Mungu katika dunia hii? Na asijue kwamba hii ni kutokana na udhaifu wetu na kutokuwa na uwezo wa uoni wetu; Mwenyezi Mungu ana pazia lake la nuru, na ikiwa Mungu angeondoa pazia hilo, uzuri wa uso wake na mwangaza wake ungeteketeza kila kitu ambacho Mwenyezi Mungu anakiona au kumuona yeye.

  1. 10- Amesema Mshairi:

Utukufu ni wake Ambaye ameweka ishara zake kwa viumbe = ili yawe wazi yaliyofichika kupitia aliyoyadhihirisha

Utukufu ni wake yule anayehuisha nyoyo za waja wake = kwa maelekezo yanayotokana na nuru yake inayowaongoza.

Hakuna zaidi baada ya kumjua Mwenyezi Mungu = ila ni kufanya yenye kuimarisha radhi zake

Wallahi hapana pa kujikinga ila kwako tu, kwani amekosa mwongozo yule ambaye hutokuwa Kimbilio Lake.

Marejeo

  1. "Kifayat al-Haja fi Sharh Sunan Ibn Majah" cha al-Sindi (1/85).
  2. Al-Bukhari (555) na Muslim (632).
  3. Majmuu’ al-Fatawa cha Ibn Taymiyyah (6/387).
  4. Al-Bukhari (247) na Muslim (2710).
  5. “Jami’ al-Ulum wa al-Hakam” cha Ibn Rajab (2/382).


Miradi ya Hadithi