عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ  قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللهِ ﷺ:«الإِيمَانُ بِضْعٌ وَسَبْعُونَ - أَوْ: بِضْعٌ وَسِتُّونَ - شُعْبَةً، فَأَفْضَلُهَا قَوْلُ: لَا إِلَهَ إِلَّا اللهُ، وَأَدْنَاهَا إِمَاطَةُ الأَذَى عَنِ الطَّرِيقِ، وَالحَيَاءُ شُعْبَةٌ مِنَ الإِيمَانِ» متفق عليه

Kutoka kwa Abu Hurayrah, (Radhi Za Mwenyezi Mungu Ziwe Juu Yake) amesema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (rehma na amani zimfikie):“Imani ina daraja sabini na kitu, au sitini na kitu.Daraja bora zaidi ni kusema: Hapana Mola apasae kuabudiwa kwa haki Isipokuwa Mwenyezi Mungu mmoja tu.Na daraja la chini kabisa ni kuondoa maudhi njiani.Na haya (aibu) ni daraja katika daraja za Imani.” Hadithi hii Imepokelewa na Imam Bukhari Na Muslimu.

Imepokewa na Al-Bukhari (9) na Muslim (35),

  1. Amesema Mtume (Rehema na Amani zimshukie) kuwa Imani ni kama mti wenye matawi ambayo mengine yako katika daraja ya juu kuliko mengine. Na Mtume, (Rehma na amani Ziwe Juu Yake) amesema kuwa imaan imegawanyika katika sehemu sabini na zaidi, na hiyo ziada ni kati ya tatu hadi tisa, hivyo ni kana kwamba alisema: Imani ni kati ya sabini na tatu hadi sabini na tisa.

Na kusema kwake: “au: sehemu sitini” ni shaka ya msimulizi, na utofauti huo katika kubainisha idadi haina shida, kwa sababu kinachokusudiwa ni kuonyesha wingi wa daraja za Imani. Baadhi ya wanazuoni wamejaribu kubainisha migawanyiko hiyo kwa kutaja matendo mema katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna za Mtume wake, na hizo ni jitihada za makadirio tu.

2.   Kisha Mtume (Rehma na amani Ziwe Juu Yake), akabainisha kuwa daraja bora kati ya hizo ni kumpwekesha Mwenyezi Mungu, nayo ni kusema Hapana Mola anaeabudiwa kwa haki Isipokuwa Mwenyezi Mungu mmoja. Na kinachokusudiwa sio kutamka tu. bali ni kuiimarisha kauli hiyo na kuifungamanisha na elimu, Yakini, ukweli, nia thabiti, upendo, utiifu, na yanayofungamana nayo, halikadhalika kukanusha kila kinachoabudiwa kinyume na Mwenyezi Mungu, na kujiepusha na ushirikina mkubwa na mdogo.

Mgawanyo huu ndio msingi wa Imani. Kwa kuwa hayatakubaliwa matendo ya mtu pasina misingi hiyo, Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema:

“Na anaye tafuta dini isiyokuwa Uislamu haitakubaliwa kwake, na siku ya mwisho atakuwa miongoni mwa walio khasirika.”

[Imran: 85].

3.   Tawi la chini kabisa kwa ubora ni kuondosha chochote kinachowadhuru watu katika njia zao; Kama vile miiba, mawe, uchafu, misumari, vitu viliyokwama, na mengineyo. ikiwa mtu ameamrishwa kuondosha madhara njiani, hata kama sio yeye aliyeweka, basi kuepuka kuweka maudhi ni jambo bora zaidi.

4.   katika daraja za Imani ni kuwa na staha (aibu), ambayo ni tabia inayohitaji kufanya Wema na kuepuka Maovu, sawa sawa Tabia hii ipo kwa mtu na akawa anadumu nayo, au hakuwa nayo hapo awali lakini akajitahidi kuwa nayo. Staha ni Tabia anayoifahamu mtu mwenyewe kwa baadhi ya nyakati, na Faida za staha ni kwamba Mwenyezi Mungu asikuone pale alipokuzuia, wala asikukose pale alipokutaka uwepo. Maelezo Yaliyotangulia yanaonyesha kwamba Imani ni kusema(kuitamka), kutenda, na kuitakidi. hivyo basi kusema “hapana Mola anaeabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu mmoja” ni kusema na kutamka kwa ulimi na kuitakidi moyoni, ikifuatiwa na kutenda kwa viungo, kwa hiyo kuondosha maudhi njiani ni katika matendo ya viungo, na staha ni katika matendo ya moyo, hata kama Athari yake inaonekana kwenye ulimi na viungo.

Mafunzo

  1. Abu Huraira (Radhi za Allah ziwe juu yake) alikuwa ni swahaba wa Mtume (Rehma na amani Ziwe Juu Yake), na mwanachuoni mkubwa, na alikuwa kiongozi katika baadhi ya Miji mikubwa, Pamoja na hayo alikuwa miongoni mwa watu wenye unyenyekevu, upole na Utiifu. Katika hili tunaweza kujiuliza “Ni kiasi gani cha unyenyekevu wetu kwa yale ambayo Mwenyezi Mungu ametupatia kama ujuzi, cheo, au mali”?

  2. Imani ni kitu kikubwa zaidi, na ndicho anachokitaka Mwenyezi Mungu kutoka kwa waja wake, na imaani ina matawi na daraja nyingi, hivyo basi kiasi gani tunajifunza daraja hizo? na ni kiasi gani tunafanya juhudi kukamilisha alichokusudia Mwenyezi Mungu katika hizo daraja? Au sisi tumelidhika na baadhi ya daraja hizo na kupuuza nyingine? 

  3. Kuna Baadhi ya watu wanaowashutumu wenzao kwa kupuuza kwao baadhi ya sehemu za Imani, na kusahau kuwa huenda wao wenyewe ni wazembe katika sehemu nyingine ya Imani, mfano kuna mtu anajitahidi katika kutekaleza ibada ya saumu na swala, na anakuwa mzembe katika kuwa na tabia njema zenye masilahi ya watu wengi. Au unakuta mtu mwingine anajitahidi katika upande wa kuwa na maadili mema na anasahau wajibu wa kuamrisha mema na kukataza maovu, yote haya yanatupeleka kuwa wapole kwa watu, na huhesabu nafsi zetu wenyewe kwa mujibu wa mizani ya kisheria, sio kama tuliyozoea.

  4. Imani ina daraja za juu na za chini, na zote Mwenyezi Mungu Mtukufu anazipenda, hivyo basi mtu asijishughulishe na ya chini kabisa akaacha ya juu, kwani katikakati ya hizo kuna daraja zaidi ya sabini, kwa hivyo bidii zetu na kutafuta kwetu daraja za juu ni jambo kubwa na bora zaidi, na pia tutambuwe hitajio letu kwa wanachuoni, na tuzidishe kutafuta elimu ya kisheria Kwa mujibu wa Kitabu cha Mwenyezi Mungu Mtukufu na Sunnah za Mtume Wake, ili tupate Kujua vipaumbele vya Sheria.

  5. Imani bora kabisa ni kusema: “hapana Mola anaeabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu mmoja” hivyo Basi tunahaja ya kujifunza maana zake, na jinsi ya kukamilisha matakwa yake, na kutamta maneno haya huku tukizijaza nyoyo zetu kwa mapenzi, unyenyekevu, na kuyakubali yote yaliyofungamana na kauli hiyo, kama vile maneno, itikadi, na matendo.

  6. Katika Kuondoa maudhi njiani yanaingia matendo mbalimbali ya watu katika maisha yao ya kila siku, ikiwemo: kuondoa kila kinachowadhuru watembea kwa miguu na magari, kama mawe, misumari, mabaki ya matairi, na mtu anaweza kuondoa mwenyewe au kuwaeleza wanaohusika kuyaondosha.

  7. Iwapo kuondoa maudhi njiani ni katika imani, basi kujiepusha kuweka maudhi njiani ni katika matendo mema, kwani kuwadhuru Waislamu na watu kwa ujumla ni katika matendo mabaya saana, na imetumika neno Maudhi hapa kwa ujumla, likijumuisha maudhi ya kihisia (yaani yanayoonekana)  kama vile kutupa mabaki ya makopo, kuweka magogo njiani, au maganda ya matunda n.k. na maudhi ya kimaana (yaani yasioyoonekana), kama vile sauti za kuudhi, harufu mbaya, na kukera watu katika namna ya kuendesha gari au kusimamisha gari katikakati ya barabara kwa muda mrefu bila sababu ya msingi, na ikiwa imekatazwa kufanya maudhi barabarani, basi ni halali kufanya kinyume chake yaani kufanya matendo mazuri, kama vile kuwarahisishia watu kwa kuweka vituo vya kupumzikia, na wepesi barabarani, kama miavuli na sehemu za kupumzikia, na hii imeashiriwa katika maneno ya Mtume (Rehma amani ziwe juu yake): “Jihadharini na kukaa njiani.” Maswahaba Wakasema: (Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu hakika sisi) Tunalazimika kukaa maeneo hayo! tukizungumza. Mtume (Rehma amani ziwe juu yake) Akasema: “Basi mkichagua kukaa mahala hapo, basi ipeni njia haki zake” maswahaba Wakauliza ni ipi haki ya njia? Mtume (Rehma amani ziwe juu yake) Akasema: “Kuinamisha macho, kujiepusha na maudhi, kuitikia salamu, kuamrisha mema na kukataza maovu”[1].

  8. Kuna malipo makubwa katika kuondosha maudhi njiani, hata kama watu hawaishi katika hizo njia, hivyo basi ni vizuri zaidi kuondoa madhara kwenye mikusanyiko mikubwa ya watu, na maeneo yao ya makazi, kama vile sehemu za kazi, na sehemu za kujifunzia, na vile vile majumbani; Na kusafisha nyumba ya familia kuna fadhila nyingi, kwa sababu ya kufanya hivyo ni kuunga udugu  na kutimiza haki zao, na kuondoa maudhi misikiti kuna fadhila nyingi zaidi, kwani ni nyumba za Mwenyezi Mungu ambazo Mwenyezi Mungu ameidhinisha ziboreshwe kwa kumtukuza yeye, hivyo basi tujitahid ibada hii iwe ndani ya maisha yetu ya kila siku.

  9. Iwapo kuondoa maudhi katika njia ni sehemu ya Imani, basi kuondosha maudhi katika nyoyo za watu ni bora zaidi, nayo ni kwa kuwaondolea ujinga, na kuwaondolea yanayowatatiza na kuzuia migongano, na kila chenye kuleta wasiwasi na huzuni kati yao.

  10. Aibu na haya ni daraja katika daraja za Imani ambalo limetajwa kwa sababu lina athari kubwa, na maana ya haya au aibu ni tabia inayokaa ndani ya nafsi na inakuwa sababu ya kupatikana tabia nyingi nzuri, na inazuia tabia mbaya, na mtu anaweza kuwa nayo bila yeye kujua, au ikapotea tabia bila kuhisi chochote, ma mara nyingi hupotea Taratibu kwa sababu ya matendo machafu, je, hili tumelizingatia? Ikiwa ndio, Je, tunaahidi kuliendeleza?

  11. Haya si tabia mbaya inayotia aibu kuifanya bali ni tabia nzuri inampelekea mtu kuacha mabaya na kufanya mema, mfano mwenye kumuonea haya Mwenyezi Mungu kwa elimu aliyompa na asisomeshe, au pesa na asizitoe katika njia yake, au hata sauti au uwezo wa kuongea na wala asiwalinganie watu kwa kutumia vitu hivyo, na aliyedhihirisha uchi anaona haya kufichua siri hiyo, au kuonekana katika dhambi, au kutenda matendo mabaya; Kama woga, ubahili na uvivu.

  12. Haya au aibu kuu zaidi ni kumuonea haya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na ukitaka kujua vizuri jambo hilo katika maisha yako basi tafakari haya maneno ya swahaba huyu aliposema: "Nakushauri umuonee Mwenyezi Mungu Mtukufu haya kama unavyomwonea haya mtu mwema unayemuhesimu".[2]

Marejeo

  1. Imepokewa na Al-Bukhari (2465) na Muslim (2121), kwa kutoka kwa Abu Saeed Al-Khudri
  2. Imepokewa na Ahmad katika Al-Zuhd (46), na Al-Bayhaqi katika Shu’ab Al-Iman (6/145) kutoka katika Hadithi ya Said bin Yazid

Miradi ya Hadithi