Aisha Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, anaripoti kuwa ufunuo na (wahyi) wa kwanza kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu rehema na amani ziwe juu yake, ulikuwa katika sura ya ndoto za kweli, Alikuwa akiona kitu katika ndoto yake, basi kinatokea kikamilifu mubashara na wazi kabisa kama nuru ya alfajiri, na hazikuwa ndoto zake kama ndoto za watu wengine, bali zilikuwa kana kwamba zinamuandaa kwa jambo kubwa. na wahyi ulianza kwa bishara njema na miuzijiza mbalimbali kama vile: kuota njozi njema, kusikia sauti za kokoto (mchanga) zikimtukuza Mwenyezi Mungu, kabla ya kuanza kulingania, kipindi hicho akiwa katika mji wa makkah, na muujiza wa jiwe kumsalimia kwa unabii na mengine mengi, yaliyolenga kumuandaa na ili ahisi ukubwa wa kile kinachokusudiwa, na ajitayarishe kwa yale yanayomngoja, na ili Malaika wasimshtue kwa yale ambayo nguvu za wanadamu haziwezi kustahimili, bali watamjia na ambayo yatautuliza moyo wake. [1]
Kisha iliingia katika nafsi yake kupenda kuwa peke yake, na kuto changanyikana na watu, na kufanya hivyo huwa kuna athari ya kuuondolea moyo wasiwasi wa kidunia, hivyo akili na tabia ya mtu vinanyooka.
Mtume (Rehema na Amani zimshukie) alikuwa akijitenga katika pango lililopo katika mlima wa Hira huko Makka, alikaa huko masiku mengi akimuabudu Mwenyezi Mungu Mtukufu. Alikuwa akitoka kwenda mlimani akiwa ameandaa chakula cha kutosha, na kinapoisha basi anarejea nyumbani kwa Bi Khadija na kuandaliwa kingine.
Wakati Mtume wa Mwenyezi Mungu (Rehma na Amani zimfikie) alipokuwa akiabudu aliteremshiwa wahyi wazi wazi, Malaika Jibril (Amani iwe juu yake), mwenye dhamana ya Wahyi akamtokea. Na kumwambia: “Soma.” Akajibu, “Mimi sijui kusoma”. Yaani: Mtume (Rehma na Amani zimfikie) alikuwa hajui kusoma wala kuandika, kama alivyosema Mwenyezi Mungu:
“Basi muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, asiyejua kusoma na kuandika.”
Mtume (Rehma na Amani zimfikie) alipomwambia kuwa hajui kusoma, malaika Jibril akamshika na kumkandamiza mpaka akachoka, kisha akamwachilia na kumwambia: “Soma.” Mtume akamjibu majibu yale ya awali, basi akamshika na kumkandamiza tena mpaka mara tatu, kisha akasema Jibril:
“Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba (1) Amemuumba binaadamu kwa tone la damu (2) Soma! Na Mola wako Mlezi ni Mkarimu kushinda wote (3) Ambaye amefundisha kwa kalamu. (4) Kamfundisha mwanadamu aliyo kuwa hayajui. (5)
Na hizi ayah za Qur`an ndizo zilikuwa ufunuo wa kwanza kwa Mtume Muhammad (Rehma na Amani zimfikie).
Baada ya hapo Mtume (Rehma na Amani zimshukie) akarejea kwa mkewe Bi Khadija Mapigo ya moyo yakienda mbio kwa sababu ya woga uliompata (kutokana na alichokiuona), akaingia ndani akamuomba Bi Khadija amfunike, kwa kawaida Mtu mwenye hofu huwa anahisi baridi kali katika viungo vyake, hivyo Bi Khadija akamfunika hadi hofu ikamtoka.
Kisha akampa khabari Mkewe na akamweleza yaliyompata kule pangoni, akamwambia: niliogopa sana. Maana yake: Aliogopa kwamba moyo wake ungepasuka kutokana na woga wake mkubwa wa kile alichokiona ambacho ni kumuona malaika Jibril akiwa katika umbile lake halisi. [2]
Bi Khadija (radhi za Allah ziwe juu yake) akamtuliza, na kusema: Wallahi, Mwenyezi Mungu hatakuchukiza, na hilo lililo kukuta si jambo baya litokanalo na shetani, Hakika ya Matendo mema ni sababu ya kumlinda mtu kutokana na maangamizi, kisha akaanza kutaja tabia zake tukufu zikiwemo: -
Kuunga udugu, kwa kuwatembelea na kuwajulia hali.
kuwasaidia wasiojiweza, ikiwemo watu dhaifi, yatima na wengineo.
Kutoa msaada wa mali kwa muhitaji,
Kuwakirimu wageni kwa kuwapa chakula na vinywaji.
Kuwasaidia watu waliofikwa na matatizo kwa misingi ya haki, sio kuwasaidia walioadhibiwa kwa uasi wao dhidi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Bi Khadija (Radhi za Allah ziwe juu yake) akampeleka kwa binamu yake Warqah bin Naufal, ambaye alikuwa ameacha ibada ya masanamu na akakubali Ukristo (halisi), na alikuwa msomi mzuri wa Taurati na injili, vilevile alikuwa anajuwa kuandika vyema lugha ya kiebrania, ambayo ndio lugha ya Wayahudi, na Alikuwa mzuri sana katika uandishi mpaka kufikia kuandika chochote alichotaka kutoka katika injili kwa lugha ya Kiebrania, pia Warqah bin Naufal alikuwa mzee sana mpaka akawa haoni.
Mtume (Rehma na Amani zimfikie) aliposimulia Waraqah bin Naufal aliyoyaona, Waraqah akamwambia kuwa yule aliyemuona ndiye Malaika mwenye siri ya Mwenyezi Mungu aliyemteremsha kwa Nabii Musa, jina lake ni Jibril (Amani iwe juu yake), alimwita hivyo kwa sababu ndio malaika pekee aliyepewa jukumu la kufikisha wahyi(ufunuo); maneno ya Waraqat bin Naufal yaliashiria kuwa Muhammad (Rehma na Amani zimfikie), atakuwa Mtume aliyetumwa na Mwenyezi Mungu kwa watu wote, kama vile Nabii Musa (amani iwe juu yake) alivyotumwa kwa Wana wa Israili.
Kisha Waraqah akaeleza kuwa watu wa Mtume watamkataa na kumpiga vita mpaka watamtoa katika Mji wake, na Waraqah alitamani kuwa laiti angelikuwa kijana wakati huo tena kijana mwenye nguvu ambaye ataweza kumtetea Mtume na kupigana vita pamoja naye, au walau angelikuwa tu hai wakati huo.
Mtume (Rehma na Amani zimfikie) alishangaa maneno ya Waraqah, na kusikitika kwa kitendo cha watu wake kumtoa katika mji wake wa Makka wakati atapokuwa akiwalingania kwenye uokovu na kumpwekesha Mwenyezi Mungu Mtukufu, hali ya kuwa Maquraishi wanaujua ukweli na uaminifu wake hapo kabla. Waraqa akamwambia kwamba ndivyo ilivyokuwa kwa Mitume wote na ndio desturi yao, na hakuna Mtume yeyote aliyekuja isipokuwa alifanyiwa uadui na kupigwa vita.
Kisha Waraqah akamwambia kuwa kama atakuwa hai wakati wa kudhihiri utume wake na kuenea dini yake, kipindi watu wake watakapomfukuza na kumkataa, basi atamsaidia msaada ulio wazi kwa kiasi atacho weza, na kwa hoja zilizo dhahiri juu ya ukweli wake na utume wake.
Kisha haukupita muda mrefu Waraqah akafariki, na wahyi ukachelewa kuteremka kwa muda.
Mtume (Rehma na Amani zimfikie) alimuoa Bi Aisha haliyakuwa ni mdogo sana: wakati alipoteremshiwa maneno matukufu mwenyezi mungu akimwambia (“Ewe Nabii! Waambie wake zako:
Ikiwa mnataka maisha ya dunia na mapambo yake, basi njooni, nitakupeni kitoka nyumba, na kukuacheni vizuri kwa wema (28) Na ikiwa mnamtaka Mwenyezi Mungu na Mtume wake na nyumba ya Akhera (pepo), basi Mwenyezi Mungu amewaandalia wafanyao mema, miongoni mwenu, malipo makubwa (29)
Mtume (Rehma na Amani zimfikie) Akamuamuru Aisha kuwauliza wazazi wake, lakini Aisha akakataa na akasema: Niwaulize wazazi wangu kwa lipi? Mimi Namtaka Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na nyumba ya Akhera”[3], wakati huo Aisha alikuwa katika umri wa ujana, hivyo akawa ni mfano wa kuigwa katika kumpa kipaumbele Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, (Rehma na Amani zimfikie).
Aisha (Mwenyezi Mungu amuwiye radhi), anaisimulia Hadithi hii, ambayo inaeleza fadhila na ubora wa Bi Khadija, ambaye alisema Aisha kuhusiana na Bi Khadija: “Sikumuonea wivu mwanamke yeyote kwa ajili ya Mtume (Rehma na Amani zimfikie), kama nilivyo muonea wivu Bi Khadija.[4]” Pamoja na hayo Wivu wake haukumzuia kusimulia hii hadithi. Na hapo tunajifunza kuwa Haifai kwa mtu kuficha sifa ya mtu au kumnyima haki yake (kwa sababu) ya kushindana naye au kuwa ni mpinzani wake, iwe katika kazi yake au katika maisha ya kila siku.
Jibril kumbana Mtume (Rehma na Amani zimfikie) na kurudia mara kwa mara neno “Soma” kunaonyesha uzuri kurudia rudia neno mpaka lieleweke kutoka kwa mhusika, na kumuandaa msikilizaji asishughulishwe na chochote kinachoweza kumsumbua na kumtoa katika malengo. Pia ili akili iwe kwa yale anayosikia, na hii ni faida kwa walinganiaji, walimu na waelimishaji; kuwaepusha watu kutokana na mambo yenye kuwatoa katika lengo la elimu yanayo athari za kusikia au kuona kwao.
Mtume (Rehma na Amani zimfikie) aliporejea kwa Bi Khadija akiwa na woga kwa yaliyompata: Bi Khadija hakubabaika wala hakuweweseka, na wala hakushughulika kumuuliza juu ya kile kilichotokea, bali aliharakisha kumfunika mpaka Mtume (Rehma na Amani zimfikie) alipotulia, na kumueleza Bi khadija hakumkanusha wala kumtuhumu akili yake, bali alimsadikisha, na akambashiria kwamba mtu mwenye sifa hizo Mwenywzi Mungu hatamfedhehesha kamwe, na alithibitisha maneno yake kwa uthibitisho huu (Hapana, wallahi, kamwe..), na akamhakikishia kwa kumtajia sifa zake nzuri, na Bi Khadija hakuridhika na hilo, bali akamchukua hadi kwa binamu yake ambaye alimfafanulia vizuri kilichotokea, na baada ya hapo Bi khadija alikuwa wa kwanza kumwamini Mtume (Rehma na Amani zimfikie), na alikuwa mfano wa mke mwema anayemsaidia mumewe na kumuondolea dhiki na taabu anapofikwa na mazito maishani.
Bi Khadija alitambua mwenendo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwamba huwasaidia wale wanaosaidia watu, hivyo hatamfedhehesha Mtume wake, hivyo basi usipoteze nguvu za kimwili, akili, pesa, na wakati, katika kufanya yasio na faida bali Wafanyieni wema watu kwa moyo mkunjufu wenye nguvu, na kutaraji malipo kwa Mwenyezi Mungu, na ukiwa katika wakati wa furaha toa na saidia watu hakika utasaidiwa katika wakati cha shida na matatizo.
zilienea kwa watu wote sifa alizojipamba nazo mbora wa viumbe, na si kwa jambo alilolifanya mara moja tu, bali ni tabia zake njema za kudumu mpaka zikageuka kuwa sifa zake mwenyewe, kama vile kuwaunga ndugu na jamaa kwa kuwatembelea, kuwasiliana nao, kutoa misaada na kudumisha kila uhusiano mzuri, na kuwa muungwana katika kuyasimamia mambo ya watu wasio weza kujifanyia mambo yao wenyewe, kama vile wanyonge, na kuwasaidia kipato cha mali au sababu zake, ikiwemo kuwapa kazi kwa wasiokuwa nazo, na kumkirimu mgeni anayepita nyumbani au mahali pa kazi, na kumsaidia kila mwenye shida.
Jambo la msingi katika kutenda wema ni kujiepusha kusifiwa na watu mbele yako, ili usijikweze na kubadilisha nia kuelekea katika mambo ya kidunia, lakini kitendo cha Bi Khadija Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, kinaonyesha kuwa inajuzu kwa mtu kumsifu ndugu yake hata akiwepo kwa manufaa, kama kumkomaza na kumuimarisha katika wakati wa mitihani, au kumpa bishara njema za matokeo ya subira yake Na mengineyo, hasa ikiwa mwenye kusifu anaamini kuwa mwenye kusifiwa hatajisikia wala kuwa na majivuno kwa maneno yake[5].
Kwa kauli ya Waraqah bin Nofal aliposema: “Hakuja mtu na mfano wa ulichokuja nacho, isipokuwa hufanyiwa uadui.” Ni Ushahidi kuwa watu hufanya uadui kwa watu wema na wanaolingania katika haki, na hili si jambo jipya. Bali ndio njia ya Mitume na wanaofanya kazi yao katika kulingania. Hivyo basi Mlinganiaji yeyote hapaswi kuacha kulingania eti kwa kuzongwa na watu waovu wakimtaka aache kulingania mema.
Mtume (Rehema na Amani zimshukie), alipenda kujitenga na kuwa peke yake kwa ajili ya kumuabudu Mwenyezi Mungu Mtukufu, na alijitenga na watu na matamanio na maneno ya dunia. Kwani kuwa peke yako wakati mwingine kuna faida, Kama hakuathiri masilahi ya watu wengine, kama mtu kuacha kazi ili kutimiza masilahi yake binafsi ya upweke, kama wanavyofanya watu wa dini potovu, au kuabudu peke yake na hiyo haitakuwa ibada sahihi