عَنْ أَنَسِ بْن مَالِكٍ رضى الله عنه، أَنَّ النَّبِيَّ ﷺ قَالَ: «العَبْدُ إِذَا وُضِعَ فِي قَبْرِهِ، وَتَوَلَّى وَذَهَبَ أَصْحَابُهُ حَتَّى إِنَّهُ لَيَسْمَعُ قَرْعَ نِعَالِهِمْ، أَتَاهُ مَلَكَانِ، فَأَقْعَدَاهُ، فَيَقُولانِ لَهُ: مَا كُنْتَ تَقُولُ فِي هَذَا الرَّجُلِ مُحَمَّدٍ ﷺ؟ فَيَقُولُ: أَشْهَدُ أَنَّهُ عَبْدُ اللَّهِ وَرَسُولُهُ، فَيُقَالُ: انْظُرْ إِلَى مَقْعَدِكَ مِنَ النَّارِ أَبْدَلَكَ اللَّهُ بِهِ مَقْعَدًا مِنَ الجَنَّةِ، قَالَ النَّبِيُّ ﷺ: فَيَرَاهُمَا جَمِيعًا، وَأَمَّا الكَافِرُ - أَوِ المُنَافِقُ - فَيَقُولُ: لا أَدْرِي، كُنْتُ أَقُولُ مَا يَقُولُ النَّاسُ، فَيُقَالُ: لا دَرَيْتَ وَلا تَلَيْتَ، ثُمَّ يُضْرَبُ بِمِطْرَقَةٍ مِنْ حَدِيدٍ ضَرْبَةً بَيْنَ أُذُنَيْهِ، فَيَصِيحُ صَيْحَةً يَسْمَعُهَا مَنْ يَلِيهِ إِلَّا الثَّقَلَيْنِ». 

Kutoka kwa Anas bin Malik Mwenyezi Mungu awe radhi naye kwamba Mtume Rehma na Amani zimshukie amesema:

“Anapowekwa mja kaburini mwake na wakageuka na kuondoka Ndugu zake, na akasikia mchakato wa viatu vyao vikigonga.Watamuijia Malaika wawili, watamkalisha, na watamuuliza: Unasemaje kuhusu mtu huyu, yaani Muhammad Rehma na Amani zimshukie?Atasema Muumini: Nashuhudia kwamba yeye ni mja wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hapo ataambiwa: Tazama makazi yako ya motoni, Mwenyezi Mungu amekubadilishia kwa kukupa makazi mazuri peponi, akasema Mtume Rehma na Amani zimshukie: ataonyeshwa makazi yote mawili.Lakini kafiri - au mnafiki - atasema: Mimi sijui, nilikuwa nikisema yale waliyoyasema watu.Ataambiwa: Hukujua wala hukusoma.Kisha atapigwa nyundo ya chuma baina ya masikio yake, na atapiga ukelele utakaosikika kwa wanaomfuatia isipokuwa watu na majini.”

  1. Mtume (rehma na amani ziwe juu yake) anawaambia maswahaba zake jambo katika mambo ya ghaibu ambayo ni Maswali ya kaburini, na neema na adhabu zake. Basi Mtume, amani iwe juu yake, anaeleza kwamba ikiwa maiti atawekwa kaburini mwake na ndugu zake wakaondoka na kumwacha huko, hurudishiwa roho yake na anaishi maisha maalum, ambayo yanayoitwa maisha ya al-Barzakh, atasikia sauti ya viatu vyao vikigonga chini wakati wa kuondoka kwao.

  2. Kisha wanamjia Malaika wawili, ikasemwa kuwa majina yao ni: Munkar na Nakeer, wanamkalisha na kumuuliza kuhusu Mtume wa Mwenyezi Mungu Rehma na Amani zimshukie anasemaje kuhusu yeye?[1] Je, alimkubali na kumuamini, na je, alitenda kwa mujibu wa sheria yake, au alimkanusha na kuifanyia mzaha dini yake?

Imetajwa katika Sunnah sahihi kwamba mja anaulizwa kuhusu Mola wake, Dini yake, na kuhusu Mtume Rehma na A mani zimshukie () kwa hiyo katika Hadithi hii imekomea kumtaja Mtume Amani iwe juu yake. Kumuamini Mtume Rehma na Amani zimshukie kunajumuisha kumwamini Mwenyezi Mungu na kukubali Uislamu kuwa dini.

3.   Iwapo mja atakuwa ni Muumini, basi atajibu kuwa Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, na kwamba anamuamini na kufuata sheria yake, basi Malaika wanambashiria Pepo. Na wanamuonyesha makazi yake katika Moto wa Jahannam alio mwandalia Mwenyezi Mungu ikiwa atakufa katika ukafiri, kisha wanamuonyesha makazi yake katika Pepo, ambayo Mwenyezi Mungu amemuandalia baada ya ukweli wa jawabu lake, na imani yake nzuri; Atakuwa radhi kwa hilo, na kaburi lake litakuwa ni uwanja mpana zaidi. 

4.   Na ikiwa maiti alikuwa ni kafiri au mnafiki na Malaika wawili wakamuuliza, basi husema: Mimi sijui, nilikuwa nikisema kama watu wanavyosema, Kafiri alikuwa akisema maneno ya makafiri: mchawi, mshairi, mwongo, mwendawazimu, na mfano wa hayo, na mnafiki alikuwa akisema maneno ya Waumini isipokuwa alikuwa akisema kwa ulimi wake na haamini anachosema kwa moyo wake na wala hamwamini Mtume Amani iwe juu yake.

5.   Malaika wawili wanamjibu kwa kumwombea dua, na wanasema: hukujua wala kumfuata mwenye kujua, wala haukunufaika na Qur’an kwa kuisoma au kuisikiliza, kwa sababu haukujishughulisha kuitafuta na kuisoma.

6.   Kisha atapigwa nyundo ya chuma kichwani, kwa pigo kali, na atapiga kelele za hali ya juu, viumbe wote watasikia kelele hiyo, isipokuwa wanadamu na majini; kwa kuwahurumia tu; Lau wangeisikia sauti hiyo, maisha yao yangeharibika, Katika Hadithi kutoka kwa Zaid bin Thabit Mwenyezi Mungu awe radhi naye kwamba Mtume, amani iwe juu yake, amesema: “Hakika Umma huu utajaribiwa katika makaburi yake, basi kama sio kuhofia kutozikana kwa kusikia adhabu za kaburini, ningemuomba Mwenyezi Mungu akusikilizisheni adhabu na mateso ya kaburini kama ninavyosikia mimi” [2] Na kwa sababu lau wangeisikia sauti hiyo, waja wangelazimika kutii na kujiepusha na maasi, na hilo ni kinyume na lengo la jaribio [3].

7.   Na adhabu ya kaburi na kuulizwa na Malaika wawili ni haki iliyothibitishwa na Qur-aan na Sunna [4], kwa hivyo Muislamu lazima aamini hivyo na wala asikanushe chochote, hata kama akili yake haiwezi kufahamu, na kunusurika kutokana na adhabu za kaburini ni bishara njema ya kuokoka Siku ya Kiyama. Yeyote atakaye nusurika katika hatua hii yanayofuata yatakuwa ni mepesi sana kwake.

Mafunzo

  1. Izoeshe nafsi yako na wengine kwa kuipa mawaidha, na uipitishe katika maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na maneno ya Mtume wake, Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ameyarahisisha kwa kuandikwa katika vitabu vilivyochapishwa, kanda za sauti na taswira, kwa hivyo basi kuwa mwenye kuikumbuka akhera kila wakati, ambayo mwanzo wake ni maisha ya kaburi, ili ujitayarishe kwa siku ya kweli. 

  2. Ukisikia khabari kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu au kwa Mtume wake, amani iwe juu yake, fikiria ni kitu gani unapaswa kufanya baada ya hayo, kuamini adhabu ya kaburi na kuulizwa maswali ya Malaika wawili kunapelekea: kujiandaa kwa ajili ya siku hiyo, kutayarisha majibu, kuharakisha kutenda mema na matendo ya utiifu ambayo yanamnufaisha mja, yanamuombea dua na kumfanya kuwa imara wakati wa kuulizwa.

  3. Hatajibu mtu kaburini isipokuwa kwa yale yaliyotulia moyoni mwake, kwani mnafiki alikuwa akirudia rudia kushuhudia kuwa Muhammad Rehma na Amani zimshukie ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, lakini hakuweza kujibu swali kaburini, kwa sababu moyo wake ulikuwa umejaa unafiki na uwongo, Hebu imarisha imani yako kwa Mwenyezi Mungu, na uwe mkweli katika kauli yako kwa kusema: Hapana Mola anaepaswa kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu mmoja, na Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu.

  4. Hana busara mwenye kuacha kuitafuta pepo pana kama mbingu na ardhi, na kujiweka mwenyewe kwenye adhabu ya kaburi na kisha kuishi milele motoni, kwa malipo ya kustarehe katika dunia kwa siku chache au miaka kadhaa, na huwenda hiyo starehe ikawa ni kwa saa chache na dakika.

  5. Muumini anaona katika kaburi lake makazi yake Peponi na Motoni, na hii ni dalili ya wazi kuwa Pepo na Moto zipo tayari zimeshaumbwa, basi jiambie kwamba Hakika huu ndio mustakbali wa maisha yangu, nimeandaa kitu gani.

  6. Kujitayarisha kwa ajili ya maswali ya kaburini na kujikinga kwa Mwenyezi Mungu na adhabu yake ni sehemu ya dini na akili ya mtu, kwani jambo lake ni kubwa, na ndio maana Mtume rehema na amani ziwe juu yake alikuwa akiomba hifadhi ya Mwenyezi Mungu katika kila sala kabla ya kutoa salam. [5]

  7. Amesema Mshairi:

Ewe Aliye Mtakatifu, hakuna Mola mlezi ila Yeye = Umetukuka ewe Mwenyezi Mungu, ambaye ni marejeo ya viumbe.

Na Ewe uliye katika Arshi juu ya viumbe vyake = Umetakasika kumpa umtakaye na kumnyima umtakaye.

Kwa Majina Yako Mazuri Zaidi na Sifa Zako Zilizo Juu = mja mnyonge anaomba Dua kwa unyenyekevu

Nataraji msaada wako juu ya kifo kichungu = wakati roho ikitolewa katika mbavu zangu.

Na uwe Rafiki mwema kimazungumzo katika giza la kaburi = utakapo rundikwa juu yangu Udongo.

Na uuthibitishe moyo na hoja yangu wakati wa kuulizwa = pale itakaposemwa: Ni nani Mola wangu Mlezi? Na wewe ulimfuata nani.

Marejeo

  1. Abu Daawuud (4753), kutoka kwa Al-Bara bin Azib.
  2. Muslim (2867).
  3. Umdat al-Qari, sherh ya Sahih al-Bukhari" na al-Ayni (8/145).
  4. Ibn al-Qattan amesema katika “Al-Iqnaa fi Masa’il Al-Ijmaa’” (1/50): “wanazuoni wa ahlu sunnah wamekubaliana kwa kauli moja kwamba adhabu ya kaburi ni kweli, na kwamba munkari na nakiri ni walaika wa makaburini na ni kweli wapo, na kwamba watu watapata mitahani katika makaburi yao baada ya kuishi humo.”
  5. Al-Bukhari (1377) na Muslim (588), kutoka kwa Abu Hurayrah


Miradi ya Hadithi