عَنْ عُبَادَةَ بْنِ الصَّامِتِ قَالَ: بَايَعْتُ رَسُولَ اللَّهِ ﷺ فِي رَهْطٍ، فَقَالَ: «أُبَايِعُكُمْ عَلَى أَنْ لا تُشْرِكُوا بِاللَّهِ شَيْئًا، وَلا تَسْرِقُوا، وَلا تَزْنُوا، وَلا تَقْتُلُوا أَوْلاَدَكُمْ، وَلا تَأْتُوا بِبُهْتَانٍ تَفْتَرُونَهُ بَيْنَ أَيْدِيكُمْ وَأَرْجُلِكُمْ، وَلا تَعْصُونِي فِي مَعْرُوفٍ، فَمَنْ وَفَى مِنْكُمْ فَأَجْرُهُ عَلَى اللَّهِ، وَمَنْ أَصَابَ مِنْ ذَلِكَ شَيْئًا فَأُخِذَ بِهِ فِي الدُّنْيَا، فَهُوَ كَفَّارَةٌ لَهُ وَطَهُورٌ، وَمَنْ سَتَرَهُ اللَّهُ فَذَلِكَ إِلَى اللَّهِ؛ إِنْ شَاءَ عَذَّبَهُ، وَإِنْ شَاءَ غَفَرَ لَهُ».

Kutoka kwa Ubaada bin As-Samit, Mwenyezi Mungu awe radhi naye amesema:

1- Niliweka kiapo cha utii kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu rehma na amani zimshukie, nikiwa katika kundi, na akasema: “Naweka kiapo cha utii kwenu kwa sharti kwamba msimshirikishe Mwenyezi Mungu na kitu chochote, msiibe, msizini, msiwaue watoto wenu. Wala msije na uwongo mnao uzua baina ya mikono yenu na miguu yenu, wala msiniasi kwa wema. 2- Na atakaye tekeleza hayo miongoni mwenu, basi ujira wake uko kwa Mwenyezi Mungu, na likimpata lolote katika hayo basi nitamuhukumu hapahapa duniani. Kufanya hivyo ndio kafara yake na inamtakasa. Na yeyote ambaye Mwenyezi Mungu atamfichia siri, basi hukumu yake ni kwa Mwenyezi Mungu. Akitaka atamuadhibu, na akipenda atamsamehe”  


1- Ubada ibn al-Samit Mwenyezi Mungu amuwie radhi anasimulia kuhusu Mtume rehma na amani zimshukie, alikula kiapo cha utii kwa makapteni wa Answaar na Khazraj kutoka kwa Ansari katika usiku wa pili wa Akaba huko Mina, wakati makapteni kumi na wawili walipotoka kwenda kwa Mtume rehma na amani zimshukie. Wakiwawakilisha walio amini katika watu wa Yathrib, Kwa hiyo Ubadah Mwenyezi Mungu amuwie radhi anataja kwamba aliweka kiapo cha utii kwa Mtume rehma na amani zimshukie akiwa katika kundi, hivyo Mtume akawawekea kiapo cha utii kwao juu ya tauhidi na kujiepusha na shirki.na wasiibe, wala wasifanye uzinzi, wala wasiue watoto wao, wala wasizuie uvumi na uwongo, na wamtii Mtume wa Mwenyezi Mungu rehma na amani zimshukie.
Na Mtume, amani iwe juu yake, alianza kwa tauhidi na kukataa ushirikina kwa sababu ndio msingi wa imani na Uislamu. Nguzo ya kwanza ya Uislamu, “hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu,” ni neno la tauhidi, na Shirki ni madhambi makubwa Zaidi. Ibn Masoud Mwenyezi Mungu amuwie radhi akasema: Nilimuuliza Mtume Rehma na Amani ziwe juu yake ni dhambi gani kubwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu? Mtume Akasema: “ Ni kumjaalia Allah kuwa ana mshirika, hali yakuwa Mwenyezi Mungu pekee ndiye aliyekuumba.”[1]   Naye Mwenyezi Mungu amefahamisha kwamba madhambi yote yamo katika matashi yake isipokuwa ushirikina.

Akasema Mwenyezi Mungu

: “Hakika Mwenyezi Mungu hasamehe kushirikishwa na kitu chochote, lakini yeye husamehe madhambi mengine tofauti na shirki tena kwa amtakaye”.

[An-Nisa: 48]


Kisha akawakataza wizi na zinaa, kwa sababu Uislamu unalinda heshima ya watu na mali, basi ikiwa watu watahalalisha uzinzi na wizi, kwa kudhulumiana wao kwa wao, wenye nguvu wakala haki za wanyonge, nasaba zikachanganyika, na watoto wa zinaa wakaenea; Ndio maana Mtume Rehema na Amani zimshukie akakanusha imani ya mwizi na mzinifu na akasema: “Mzinifu hafanyi zinaa hali ya kuwa ni Muumini, na mwizi haibi akiwa ni Muumini, Wala hanywi mvinyo na hali yeye ni Muumini.” [2] 
Waarabu walikuwa wakiwauwa watoto wao kwa sababu ya umasikini wao, au kwa kuhofia kuwa watakuwa masikini kwa ajili yao, basi Mwenyezi Mungu akawakataza hayo kwa kusema:

“Wala msiwauwe watoto wenu kwa sababu ya umasikini. Sisi tunakuruzukuni nyinyi na wao”. 

[Al-An’am: 151]

Hali hii inatokana na masikini anayemuua mwanawe kwa ajili ya umasikini wake

na akasema Mwenyezi Mungu:

Wala msiwauwe watoto wenu kwa kuogopa umasikini. Sisi tunawaruzuku wao na nyinyi.” .

[Al-Isra: 31, 32]

Na dalili hii ni kwa mtu anayemuua mwanawe kwa kuhofia kuwa umaskini utamkumba. Na miongoni mwao walikuwa wakiwazika mabinti zao wakiwa hai kwa kuogopa fedheha.

Kisha Mwenyezi Mungu akasema:

“Na msichana aliye zikwa hai atapo ulizwa (8) Kwa kosa gani aliuliwa” .

[Al-Takwir: 8, 9]


Na Mtume, amani iwe juu yake, akawakataza kuzusha uwongo na kuwatuhumu watu kwa uwongo, ambayo ni pamoja na kutoa ushahidi wa uwongo, kuwasingizia Waumini wanaume na Waumini wanawake, na kuwasengenya kwa wasiyohusika nayo, na ushahidi wa hayo kauli yake

Mtume amani iwe juu yake:

"Je, unajua kusengenya ni nini?" Wakasema Maswahaba: “Mwenyezi Mungu na Mtume wake ndio wanajua zaidi.” Akasema Mtume: “Ni kumsema Ndugu yako kwa yale anayoyachukia.” Ikasemwa: Je! Unaonaje Kama ninayoyasema yakiwa kweli? Akasema Mtume: “Ikiwa mnayosema anahusika nayo, basi mnakuwa mmemsengenya, na ikiwa hahusiki nayo, basi mmemzushia. [3] 

2- Kisha Mtume akawaeleza kwamba yeyote miongoni mwao atakayekuwa na msimamo juu ya yale aliyoyaahidi, basi atapata ujira kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ambao ni radhi zake Mwenyezi Mungu, na kuingia pepni.

“Bila ya shaka wanao fungamana nawe, kwa hakika wanafungamana na Mwenyezi Mungu. Mkono wa Mwenyezi Mungu uko juu ya mikono yao. Basi avunjaye ahadi hizi anavunja kwa kuidhuru nafsi yake; na anaye tekeleza aliyo muahadi Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu atamlipa ujira mkubwa”.

[Al-Fath: 10]

Na mwenye kutenda dhambi yoyote aliyoiharamisha Mwenyezi Mungu ambayo itamwajibisha kuadhibiwa hadd, basi ataadhibiwa hapa duniani, na itakuwa ni utakaso wa nafsi yake kutokana na dhambi na adhabu yake itaondolewa Akhera. Yeyote atakaye adhibiwa adhabu ya zinaa, wizi, unywaji pombe, kashfa na mengineyo katika dunia. Hataadhibiwa akhera. Na atakayefichwa na Mwenyezi Mungu na akawa hakuadhibiwa hapa duniani, basi hukumu yake ni kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu; Akitaka atamuadhibu kwa dhambi hiyo, kisha atamuingiza Peponi, na akitaka atasamehewa.


1- (1) Tawhid ni ibada kubwa kabisa ambayo kwayo mtu hujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, na kwa ajili hiyo ndio maana ikawa “ukumbusho bora zaidi ni hapana Mola ila Mwenyezi Mungu mmoja tu”[4]   na ushirikina ni madhambi makubwa zaidi, na ni dhulma kubwa ambayo Mwenyezi Mungu haisamehe. Kila Muislamu lazima arekebishe tauhidi yake ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na aisafishe kutokana na ushirikina hata kama ni mdogo.


2- Mtume, Rehma na Amani ziwe juu yake, alianza na lililo muhimu zaidi, kisha lililo muhimu zaidi. Mlinganiaji, Msomi, na Mwalimu anapaswa kuwa makini na mambo muhimu zaidi, na kuyatanguliza kuliko mengine.


3- 2-(1) Muumini kamwe haibi, wala hatazami asichokuwa nacho, bali anajua kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu amegawanya riziki kwa hekima yake, na kwamba riziki yake imeandikwa kwenye Ubao Uliohifadhiwa kabla ya Mwenyezi Mungu kuumba mbingu na ardhi.

4- (1) Muumini anajua kwamba Mwenyezi Mungu atamwajibisha kwa fedha zake; Alipata wapi na aliitumiaje? Ndio maana yuko mbali zaidi na kuchukua pesa za watu bila haki.

5- (1) Muumini aepuke zinaa; Anajua kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu ameharamisha zinaa, na ameifanya kuwa ni dhambi kubwa, kutoka kwa Abdullah bin Masoud

Mwenyezi Mungu amuwie radhi amesema:

Nilimuuliza Mtume rehma na amani zimshukie: Ni dhambi gani kubwa zaidi? Akasema: KuMuabudu  pamoja naye mungu mwingine, hali yakuwa Mwenyezi Mungu mtukufu pekee ndiye aliyekuumba. Nikasema: Hilo ni kubwa.” Nikasema: Kisha lipi? Akasema: kumuua mtoto wako kusudi asile nawe pamoja” nikasema: kisha lipi? Akajibu “Kumzini mke wa jirani yako” [5]

  Na uthibitisho wa hayo unatokana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu aliposema:

“Na wale wasio mwomba mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu, wala hawaui nafsi aliyo iharimisha Mwenyezi Mungu isipo kuwa kwa haki, wala hawazini - na atakaye fanya hayo atapata madhambi (68) Atazidishiwa adhabu Siku ya Kiyama, na atadumu humo kwa kufedheheka”.

[Al-Furqan: 68, 69]


6- (1) Kuua Nafsi ni kosa kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na amemuahidi muuaji adhabu kali kabisa.

Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

“Na mwenye kumuuwa Muumini kwa kukusudia, basi malipo yake ni Jahannamu humo atadumu, na Mwenyezi Mungu amemkasirikia, na amemlaani, na amemuandalia adhabu kubwa” .

[An-Nisaa: 93]

Haijuzu kwa Mwislamu kumwaga damu za watu isivyo halali, na haifai kwa mtu mwenye akili timamu kufanya mauaji wakati anaijua adhabu hii chungu inayomngoja huko Akhera.

7- (1) Kumwamini Mwenyezi Mungu Mtukufu na kuridhika na amri yake ndio msingi wa furaha na faraja katika ulimwengu huu; Laiti mtu angelijua kwamba riziki yake iko mikononi mwa Mwenyezi Mungu, basi idadi kubwa ya watoto isingemuathiri au upungufu wa watoto, na moyo wake ungalitulia na kustarehe, na hasumbuki na idadi kubwa ya watoto wake. Ukiachilia mbali kuwaua kwa umasikini.

8- Ikiwa kuua ni dhambi kubwa, basi kuua watoto ni kosa kubwa zaidi. Kwakuwa Inajumuisha kukata uhusiano wa kindugu, uchungu kati ya familia, uharibifu wa nyumba, pamoja na kumdhania vibaya Mwenyezi Mungu.

9- Kuzusha uvumi, kuzizua na kuzieneza bila ya kuwa na yakini nazo ni kinyume cha Dini iliyo sawasawa, na ndio maana Mwenyezi Mungu Mtukufu akatukataza na akasema:

“Na kwa nini mlipo yasikia msiseme: Haitufalii kuzungumza haya. Subhanak Umetakasika! Huu ni uzushi mkubwa (16) Mwenyezi Mungu anakuonyeni msirejee tena kufanya kama haya kabisa, ikiwa nyinyi ni Waumini”

[An-Nur: 16, 17]

Na akawaahidi wafanyao fitna kwa kusema kwake mtukufu:

“Kwa hakika wale wanao penda uenee uchafu kwa walio amini, watapata adhabu chungu katika dunia na Akhera” .

[An-Nur: 19]


10- Mtume rehma na amani zimshukie ameweka ukomo wa kumtii katika mema, ingawa Mtume, amani iwe juu yake, haamrishi isipokuwa ni mema tu; Ili iwe ndio msingi katika ibada zote; Haijuzu kumtii mtu ye yote, awe mzazi, mlezi, au mfano wa hayo - isipokuwa katika mema.Hakuna kumtii kiumbe katika kumuasi Muumba.

11- Kutekeleza adhabu ya hadd ni kafara kwa mhusika, haijuzu kwa Muislamu kumtukana mtu aliyepatilizwa adhabu ya hadd. Khalid, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, alipomtukana yule mwanamke ambaye alitekelezewa adhabu yake, Mtume rehma na amani zimshukie akamwambia:

“Ngoja Khalid, Naapa kwa Yule Ambaye nafsi yangu imo Mikononi Mwake, hakika ametubia toba ambayo angelitubia mtoza ushuru wa ukandamizaji angesamehewa.” [6] 

12- Jua kwamba haki za watu hazipotei kwa kutubia tu, bali mpaka mali zilizodhulumiwa zirudishwe kwa watu wao, basi jihadhari na kujiepusha na madhambi ya watu kabla ya kuridhiana kwa matendo mema na mabaya.

13- Inastahiki kwa Muislamu, ikiwa amefanya dhambi, ajifiche na atubie kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na asijitokeze kwenye kuanzishwa kwa adhabu ya hadd na kuingia katika kashfa; Maaiz alikuja kwa Abu Bakr as-Siddiq, Mungu awawie radhi, na akamwambia kwamba amezini, basi Abu Bakr Mwenyezi Mungu awe radhi nao wote wawili akasema: Je, umemweleza yeyote asiyekuwa mimi? akasema hapana. Akasema Abu Bakr: Basi tubu kwa Mwenyezi Mungu na jifunike pazia la Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anapokea toba za waja wake, lakini Maaiz hakuiridhia hiyo hukumu mpaka alipomjia Umar bin Al-Khattab na kumwambia kama alivyosema Abu Bakr, lakini hakuikubali mpaka akamuendea Mtume wa Mwenyezi Mungu Amani iwe juu yake, hapo mtume akamtekelezea adhabu ya had ya zinaa juu yake [7].

Marejeo

  1. Imepokewa na Al-Bukhari (4477) na Muslim (86).
  2. Imepokewa na Al-Bukhari (2475) na Muslim (100).
  3. Imepokewa na Muslim (2589).
  4. Imepokewa na Al-Tirmidhiy (3383) na Ibn Majah (3800).
  5. Imepokewa na Al-Bukhari (4477) na Muslim (86).
  6. Imesimuliwa na Muslim (1695).
  7.  Imepokewa na Al-Nasa’i katika Al-Sunan Al-Kubra (16999), kwa kutoka kwa Said bin Al-Musayyib, Mwenyezi Mungu amrehemu.


Miradi ya Hadithi