عَنْ عُمَرَ بْنِ الخَطَّابِ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللهِ ﷺ: «إِنَّمَا الْأَعْمَالُ بِالنِّيَّةِ. وَإِنَّمَا لِامْرِئٍ مَا نَوَى. فَمَنْ كَانَتْ هِجْرَتُهُ إِلَى اللهِ وَرَسُولِـهِ، فَهِجْرَتُهُ إِلَى اللهِ وَرَسُولِـهِ. وَمَنْ كَانَتْ هِجْرَتُهُ لِدُنْيَا يُصِيبُهَا، أَوِ امْرَأَةٍ يَتَزَوَّجُهَا، فَهِجْرَتُهُ إِلَى مَا هَاجَرَ إِلَيْهِ» متفق عليه.

Kutoka kwa Umar bin Al-Khattab, (r.a) amesema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.).

1. Hakika matendo huhesabika kwa nia tu. 

2. Na hakika kila mtu atalipwa kwa alilokusudia. 

3. Basi atakaekuwa kuhama kwake ni kwa ajili Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi kuhama kwake ni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. 

4. Na atakayekuwa kuhama kwake ni kwa ajili ya dunia ili aipate, au mwanamke ili amuoe, basi kuhama kwake ni lile aliloliendea.” (Imepokelewa na Imam Bukhari na Muslimu).


Hadithi hii ni moja ya hadithi muhimu katika dini nzima, mpaka Wanazuoni wakasema: Hadithi hii inawakilisha theluthi moja ya Uislamu.[1]

1- Kwa nia, matendo yanapata sifa kubwa, na nia ni makusudio amabayo moyo umeelekea kwake, na kuyakusudia kwa vitendo vyake, kwa hivyo ibada zinatofautishwa na mazoea, na aina za ibada zinatofautiana. matendo yanakubaliwa ikiwa ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kinyume na hapo hukataliwa.

2- Ikiwa atakusudia jambo zuri basi atalipwa zuri, na ikiwa atakusudia jambo baya ataadhibiwa, na ikiwa hajakusudia chochote basi hana thawabu wala thambi, bali hutofautiana daraja za matendo kulingana na daraja za nia.
Matendo yanaweza kushabihiana na makusudio yakawa tofauti, na hakika kila mtu hulipwa kulingana na kitendo alichokusudia.

Nia njema haisahihishi kitendo kiovu. Kuna baadhi ya watu walizua njia haramu ya nyiradi. Abdullah bin Masoud (r.a) alipowakemea, walisema: Wallahi, ewe Abu Abd Al-Rahman, sisi tulikuwa tunakusudia kufanya mema tu. Akasema: "Ni watu wangapi wanaokusudia mema na hawapatii[2]".

3- Kisha Mtume (s.a.w) akalifafanua suala hili, na akatoa mfano wa hilo kwa kuhama (ambako ni kuiacha sehemu ya ukafiri na kuelekea sehemu ulipo Uislamu) ; Yeyote aliyehama kwa Mwenyezi Mungu; kwa kutakasa nia katika hilo na katika hali ya kumuabudu yeye pekee, na kuhama kwake kukawa ni kwa ajili ya  Mtume (s.a.w) hali ya  kunyenyekea  na kutii amri yake, na kufuata muenendo wake, huo ndio uhamaji halisi unaostahiki kutajwa na kutukuzwa. .
Na Mtume (s.a.w) hakutaja malipo hapa katika kuheshimu ujira huu, kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu alificha malipo ya saumu pale aliposema katika hadithi Qudsi: “Kila matendo ya mwanadamu ni yake. Isipokuwa saumu, kwani ni kwa ajili Yangu na mimi nina malipo yake[3]”.

4- Na mwenye kuhama kwa ajili ya malengo ya kidunia - kama biashara au mwanamke - basi kuhama kwake hakuchukuliwi kuwa ni halali na wala hapati thawabu kwa hilo, ingawa kuhama ni miongoni mwa vitendo vikubwa vya utiifu. vivyo hivyo ibada nyingine zote - na kuhama kwake kunahusishwa tu na kazi aliyoikusudia.
Mtume (s.a.w) hakutaja kuwa ana malipo, kwa sababu makusudio yake si ibada safi, na watu wanakhitalifiana katika lengo hili.


1- Sahihisha nia yako, na uchunge moyo wako, na jitahidi kufanya matendo yako yote kwa ajili ya utii kwa Mwenyezi Mungu. Mtume, (s.a.w) anasema: “Mwenyezi Mungu haangalii sura zenu wala mali zenu; bali anaangalia nyoyo zenu na vitendo vyenu.”
2- Usidanganywe na mwonekano wa dhahiri wa matendo yako, au matendo ya wengine wenye imani mbaya, kwani matendo yamefungamana na nia.
3- Kithirisha nia njema, kwani nia ya Muumini ni kubwa zaidi kuliko kitendo chake, kwa sababu akikusudia kufanya jambo jema atalipwa thawabu, iwe amefanya au hajafanya, Mtume (s.a.w).

alisema wakati anarudi kutoka kwenye vita vya Tabuk:

(Hakika katika mji wa madina tumewaacha watu, hampigi hatua , wala kulivuka bonde, bali wapo pamoja nanyi.” Wakasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, inakuwaje hali ya kuwa  wapo katika mji wa Madina? Akasema: “, wapo madina lakini wamezuiliwa na udhuru katika kuwa nasi”[4] )

na katika Hadithi nyingine Mtume anasema :

  «…..Mtu ambaye Mwenyezi Mungu amempatia mali na elimu, akawa anafanyia kazi elimu yake na mali yake katika njia sahihi, na mtu ambae Mwenyezi Mungu amempatia elimu tu bila mali, akawa anasema laiti ningelikuwa kama Fulani ningelifanya kama anavyofanya , basi wote wawali katika malipo wapo sawa…[5]»


4- wema waliotangalia, Mwenyezi Mungu awawie radhi, walikuwa wakijifunza nia - kwa ufuatiliaji, adabu, na kulenga mema - kama walivyojifunza kufanya kazi. Yahya bin Abi Katheer amesema: “Jifunzeni nia; kwani nia Inaelimisha zaidi kuliko vitendo.” Sufyan al-Thawri amesema: “Sijashughulikia jambo lolote kali kuliko ya nia yangu. Kwa sababu inanibadilikia badilikia.[6]” 

5- Kwa nia, mazoea yanageuzwa kuwa matendo ya ibada. Mtu akila anakusudia kuutia nguvu mwili wake katika utiifu, ibada na matendo mengine, na akifanya kazi au mfanyabiashara huku anakusudia kuimarisha ardhi, kuwanufaisha Waislamu, na kukusanya pesa anazozitumia kwa familia yake kwa halali, na akitafuta elimu anakusudia kunufaisha nafsi yake na watu wengine kwa kufuata njia ya manabii na wanazuoni, na akitaka kulala anakusudia kuupumzisha mwili wake ili aweze Kuendelea kufanya kazi na ibada, basi atalipwa. kwa hayo yote. Amesema Muadh bin Jabal, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi: “Mimi nalala na kuamka, basi natarajia malipo katika usingizi wangu, kama ninavyotaraji malipo ya kisimamo changu.

6- Iwapo utafanya kazi ya lazima, basi weka nia ya kuMuabudu  Mwenyezi Mungu ndani ya kazi hiyo, Zubaid Al-Yamami amesema: “Mimi Napenda kuwa na nia katika kila jambo, hata katika chakula na kinywaji chake”., Abdullah bin Al-Mubarak alisema: “Huenda amali ndogo ikakuzwa kwa nia, na pengine amali kubwa ikafanywa kuwa ndogo kwa nia.

7- Zinduka, na jiepusheni na viingilio vya Shet'ani kwa kupotosha ibada yako kwa kufanya ibada kwa ajili ya kuonwa au kusifiwa na watu, na kuwatukuza, ukifanya hivyo utapata hasara.,

akasema Mtume (s.a.w) katika hadithil Quds:

"Mwenyezi Mungu mtukufu amesema: mimi nimejitosheleza kuwa na washirika (atake tenda kitendo akawa amenishirikisha na chochote ndani yake, nitamuacha na huyo mshirika wake. [7]

8- Unganisha kati ya nia njema na kumfuata Mtume (s.a.w)  kwani huo ndio uhalisia wa kuhamia kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake (s.a.w). Amesema Al-Fudayl bin Iyad katika kauli ya Mola Mtukufu aliposema:

“Ambaye ameumba mauti na uhai ili kukujaribuni ni nani miongoni mwenu mwenye matendo mazuri Zaidi).”

(Mulk:02)

Matendo mazuri Zaidi ina maana ya matendo yalivyo sahihi zaidi na yenye nia ya kumkusudia Mwenyezi Mungu peke yake, na yalivyo sahihi zaidi katika  kupatia kufuata mwenendo wa Mtume (s.a.w), kwani matendo yatakapokuwa ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu yakakosa kufuata  mwenendo wa Mtume (s.a.w) hayatakubaliwa. Na mtendaji amepatia katika kufuata mwenendo wa Mtume (s.a.w) akakosa kufanya kwa ajili ya Mwenyezi Mungu basi hatokubaliwa

9- Mshairi amesema:
Ukitaka uitwe mkarimu, mstaarabu = mchamungu, msiri, mtukufu, mwenye akili huru
Basi kuwa mwenye kufanya kwa ajili Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka,, na kuwa mfuasi wa Mtume (s.a.w), utapata malipo.

Marejeo

  1. “tazama kitabu cha “sherhe ya Arubaini Al-Nawawi” cha Ibn Daqiq Al-Eid” (uk.: 24), na “Jaami’ Al-Uloom wa Al-Hakam cha Ibn Rajab” (1/71)
  2. Sunan al-Darami (210).
  3. Al-Bukhari (5927), na Muslim (1151).
  4. Muslim (4423).
  5. Ahmad (18024) na Ibn Majah (4228).
  6. Jaami Al Ahkami Wal Hikam Ya Ibun Rajab 1/70
  7. Muslim (2985).


Miradi ya Hadithi