عن أبي هُرَيْرَةَ رضي الله عنه، قال:سَأَلَ رَجُلٌ رَسُولَ اللهِ ، فَقَالَ: يَا رَسُولَ اللهِ، إِنَّا نَرْكَبُ البَحْرَ، وَنَحْمِلُ مَعَنَا القَلِيلَ مِنَ الْمَاءِ، فَإِنْ تَوَضَّأْنَا بِهِ عَطِشْنَا، أَفَنَتَوَضَّأُ مِنَ الْبَحْرِ؟ فَقَالَ رَسُولُ اللهِ : «هُوَ الطَّهُورُ مَاؤُهُ، الحِلُّ مَيْتَتُهُ»

Kutoka kwa Abu Hurayrah, Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake  amesema:

1.mtu mmoja alimuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu (Rehma na amani ziwe juu yake) akasema: “ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, sisi husafari safari za baharini, na katika safari zetu hubeba maji machache, ikiwa tutayatumia kupata udhu basi tutapata kiu – kwa kukosa maji ya kunywa- je inafaa tupate udhu kwa maji ya bahari? 

2. akasema Mtume wa Mwenyezi Mungu rehema na amani ziwe juu yake: “maji yake ni twahara”. 

3. na kilichofia baharini ni halali"

1. Mtu mmoja miongoni mwa Maswahaba, Mwenyezi Mungu awawie radhi, alimuuliza Mtume Rehema na Amani zimshukie kuhusu kutawadha kwa maji ya bahari; kwani wengi wao walikuwa wakisafiri baharini na kubeba maji kidogo, ikiwa watayatumia kutawadha basi watapatwa na kiu kwa kukosa maji safi ya kunywa, wakauliza je, inajuzu kwao - katika hali hii - kutawadha kutokana na maji ya bahari?

2. Mtume (rehema na amani ziwe juu yake) akajibu kuwa maji ya bahari asli yake ni safi na yanaweza kusafisha kitu kingine, hata ikiwa rangi na ladha yake ni tofauti na maji mengine matamu.

3. Mtume akumuongezea faida kwa kumbainishia kwamba mnyama yeyote katika wanyama wanaoishi baharini, basi inafaa kumla, ispokuwa wale waliotolewa katika hukumu hiyo, kama Mwenyezi Mungu alivosema:

" Mmeharamishiwa nyamafu,"

[Al-Ma’idah: 03].

Na mtume amesema:

" Mmehalalishiwa -kula aina mbili za visivyochinjwa- na damu mbili, ama aina mbili za visivyochinjwa ni nyangumi na nzige, na damu mbili ni ini na bandama.[1]"

MAFUNDISHO:

1.Swali la swahaba  lilikuwa wazi, kwani alielezea msimamo wake kikamilifu; Kwa sababu fat-wa inaweza kutofautiana kulingana na hali na eneo, hivyo basi muulizaji ni lazima amuelezee kwa uwazi kabisa suala lake mbele ya mufti, na mufti asijibu mpaka aelewe suala hilo kikamilifu kwa vipengele vyake.

2.Swahaba  huyu alikuwa anapenda sana mambo ya Dini yake, ingawa alikuwa msafiri anayeweza kuunganisha Swala au kuchelewesha Swalah mpaka mwisho wa wakati wake hadi awasili eneo anakoenda ikiwa safari yake ni fupi, lakini yeye alipenda kuuliza masuala haya, kwa kutilia maanani utendaji wa kuswali swala kwa wakati. Hivyo basi Hatupaswi kujishughulisha na mambo ya kidunia badala ya kuMuabudu  Mungu Mwenyezi.

3. Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, akajibu kwa kusema: “Ni maji safi,” na hakujibu “ndiyo,”; ili isije ikafahamika kwamba inajuzu kwa mtu kutawadha maji ya bahari pale tu anaposafiri baharini na maji kidogo, na haijuzu kuosha uchafu na maji hayo. Bali alisema: “Ni maji safi” ili kuonyesha hukumu ya jumla kwamba maji ya bahari ni safi na yanatwaharisha, sawa iwe kuna maji mengine safi au la, na sawa ikiwa mtu yuko safarini au mkaazi[2] na hii inaonesha upeo katika hekima ya mwanasheria; kwani Jibu lake linapaswa kuwa wazi na lisiwe na dhana.

4.Kauli ya Mtume (rehema na amani ziwe juu yake): “Ni maji safi,” kwa kubainisha maneno hayo mawili ni uthibitisho wa hukumu; Angeweza kusema: maji ya bahari ni safi, lakini alithibitisha hilo kwa kufafanua maneno yote mawili. Hivyo basi ni lazima kwa mwanachuoni na msomi wa sheria majibu yake yawe yana uhakika na hakuna nafasi ya shaka ndani yake, vinginevyo muulizaji atabaki na sintofahamu katika kufanya kazi na fat-wa.

5. Katika hii Hadith, inajuzu kuongeza katika jibu la muulizaji kwa jambo ambalo hakuuliza, ikiwa muulizwaji ataona haja ya muulizaji kwa kile ambacho hakikuwa katika swali; Kwani muulizaji katika hadithi hii alikuwa akisafiri baharini mara kwa mara, na hili lilimlazimu kukutana na samaki waliokufa wakielea juu ya maji, basi Mtume (Rehema na amani ziwe juu yake) akamjulisha kuwa ni halali na inajuzu kwake kula. Hvyo basi Ni bora kwa mlinganiaji,na mwalimu na msomi wa sheria asitosheke kujibu swali la muulizaji kwa yale yaliyojumuishwa katika swali lake, ikiwa anaona kitu kingine kinachohusiana nayo ambacho muulizaji amesahau kuuliza juu yake basi yeye aongezee ili kutoa faida zaidi.[3]

Marejeo

  1. Imepokewa na Ibn Majah (3314).
  2. "Nail al-Awtar" cha al-Shawkani (1/29, 30).
  3. "Nail al-Awtar" cha al-Shawkani (1/30, 31).


Miradi ya Hadithi