2 - KUSHUHUDIA KUWA HAPANA MOLA APASAE KUABUDIWA KWA HAKI ISPOKUWA ALLAH:

عَن مُعاذِ بنِ جبلٍ ‏‏رضى الله عنه قال:كنتُ رَدِيفَ النبيِّ ﷺ على حمارٍ، فقال: «يا معاذُ!، أتدري ما حقُّ اللهِ على العبادِ؟ وما حقُّ العبادِ على اللهِ؟» قلتُ: اللهُ ورسولُه أعلمُ. قال: «فإنَّ حقَّ الله على العبادِ أن يعبدوه ولا يُشركوا به شيئًا.وحقَّ العباد على الله أن لا يُعذِّب مَن لا يُشرك به شيئًا».قلتُ: يا رسول الله، أفلا أُبشِّر الناس؟ قال: «لا تُبَشِّرْهم فيتَّكلوا» متفق عليه.

Kutoka kwa Mua’dh ibn Jabal (r.a) amesema:

1. Nilikuwa nimepanda nyuma ya Mtume (s.a.w) katika mnyama. 

2. Akasema Mtume (s.a.w): “ewe Mua’dh! Je, wajuwa ni ipi haki ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake? na ni ipi haki ya waja kwa Mwenyezi Mungu”?  3.Nikasema: Mwenyezi Mungu na Mtume wake ndio wajuzi zaidi juu ya hilo. 4.Akasema Mtume (s.a.w): “hakika haki ya Mwenyezi Mungu juu ya waja wake ni kumuabudu yeye peke yake wala wasimshirikishe na chochote 5. Na haki ya waja juu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ni kutomuadhibu yeyote asiemshirikisha na chochote” 

6.Nikasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, je nisiwabashirie watu? Akasema Mtume rehma na amani ziwe juu yake: “Hapana usiwape bishara hii, kwani watakuwa wavivu”

  1. Alikuwa Mua’dh amepanda nyuma ya Mtume (s.a.w) juu ya punda.

  2. Akataka Mtume rehma na amani ziwe juu yake kubainisha mafunzo yake, akamuuliza: Je ni yapi anayostahiki Mwenyezi Mungu Mtukufu, juu ya waja wake miongoni mwa yaliyo wajibu kwao? na nizipi haki za waja ambazo ameziwajibisha juu ya nafsi yake?

  3. Mua’dh (r.a) akajibu kwa kusema “Mwenyezi Mungu na Mtume wake ndio wajuzi zaidi juu ya hilo”, yaani: mimi sijui. na mfano wa maneno haya husemwa katika mambo ya kisheria, lakini akiulizwa mtu kunako mambo ya kidunia, au mambo yaliyofichikana na mengineyo miongoni mwa asiyo yajuwa Mtume (s.a.w) basi aseme “Mwenyezi Mungu ndio mjuzi zaidi”.

  4. Basi Mtume (s.a.w) akabainisha jawabu; akasema kuwa haki ya Mwenyezi Mungu –mtukufu - kwa waja wake waelekee kwake kwa kumuabudu, na ibada, Maana yake ni:  jina lililokusa kila anachokipenda Mwenyezi Mungu  mtukufu na anakiridhia, katika maneno na vitendo vya wazi na vya siri  [1], nayo ni hali ya kujidhalilisha na kutii na kuelekea moyo kwa anaestahiki kuabudiwa, na nilazima pamoja na kumuabudu Mwenyezi Mungu [2] wasimshirikishe na yeyote katika ibada yake- hata akiwa nabii ( alipewa ufunuo) au malaika au mja mwema- wala kwa aina yeyote ya ushikina- hata ikiwa ndogo kiasi gani, japo hata kwa kutamka tu, basi hii ndio haki ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake:

    “Na amekwisha toa hukumu mola wako kwamba msiMuabudu  yeyote isipokuwa yeye peke yake”

    [al-israai:23]

    na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

    “Na sikuwaumba majini  na watu isipokuwa waniabudu mimi peke yangu (56)mimi sihitaji kutoka kwao riziki wala chakula (57) hakika Mwenyezi Mungu ndio mtoaji wa riziki zote tena mwenye nguvu Madhubuti ”

    [adh-dhariyat:56-58].

  5. Na haki za waja kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ni haki ameiwajibisha Allah mtukufu juu ya nafsi yake kwa ukarimu tu kutoka kwake, na haikuwa wajibu kwake [3] kwamba wao ikiwa watamuabudu na wasimshirikishe na chochote, asiwaingize motoni basi “ mwenye kukutana na mola mtukufu ilihali hamshirikishi na chochote katika ibada ataingia peponi, na atakaekutana na Mwenyezi Mungu haliyakua ni mshirikina ataingia motoni” [4]

    “ Hakika mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu basi Mwenyezi Mungu ameiharamisha pepo kwake, na mafikio yake itakua ni motoni na watu waovu hawana atakae wanusuru na kuwaokoa ”

    [al-maidat:72].

     Na maana ya hayo ni kwamba muislamu mwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu Mtukufu, hatoishi motoni milele, na ikiwa mema yake yatakuwa zaidi kuliko maasi ataingia peponi na ataharamishiwa moto, na ikiwa ni katika waasi na maasi yakawa mengi zaidi basi hukumu yake inabaki kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, akitaka atamuadhibu atakavyo kisha amuweke peponi, na akitaka anamsamehe na anamuingiza peponi. Ama aliyekufa katika ushirikina, hahika hatoingia peponi, bali ataishi motoni milele na milele pasina kikomo cha adhabu.

    “Hakika Mwenyezi Mungu hamsamehe mwenye kumshirikisha bali anasamehe tofauti na shirki kwa amtakae, na yeyote mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu basi anakuwa amezusha madhambi makubwa”

    [an-nisaa:48][5] .


  6. Aliposikia Mua’dh hiyo bishara njema kutoka kwa Mtume Muhammad (s.a.w) alipenda awabashirie watu, lakini akaomba ushauri kwa Mtume (s.a.w), na Mtume akamshauri kuwa asifanye hivyo, kwa sababu baadhi yao, huwenda watakapo yajua hayo watabweteka kwenye kumpwekeshaMwenyezi Mungu Mtukufu, na watakuwa wavivu wa kufanya ibada na utiifu na wataacha kabisa. Na zimekuja hadithi zingine zikiashiria kwamba Mua’dh (r.a) alifahamu kuwa katazo la Mtume lilimaanisha wosia kwa maslahi ya kuto kubweteka na kwamba jambo hilo sio kosa kulizungumza kwa masilahi ya taaluma na mengineyo, na kwa ajili hiyo Mua’dhi Alisimulia watu karibu na kifo kwa kuhofia kupata madhambi ya kuficha elimu.

Mafunzo

  1. Usifanye jeuri kwa kutopanda kipandwa ambaco sio cha kifakhari, na ichunguze nafsi yako wakati inapo kataa kuchanganyika na tabaka tofauti za watu, au kula nao, ni katika mambo yanayoashiria kiburi cha wazi kabisa au jeuri iliyo jificha, na hakika Mtume (s.a.w) alipanda punda, na akapanda Mua’dh nyuma yake, naye Mtume rehma na amani ndio kiigizo chetu katika unyenyekevu, na kuchangamana na watu.

  2. Usijizuie kunufaika kwa vitu alivyo vidhalilisha Mwenyezi Mungu Mtukufu katika wanyama, na utumie vitu hivyo kistaarabu, kwa hakika alipanda Mtume Muhammad (s.a.w) yeye na Mua’dh juu ya mnyama mmoja.

  3. Alitumia Mtume (s.a.w) njia ya kuuliza katika kumfundisha Mua’dh (r.a); ili kumuhimiza kuitumikisha akili, na ili lipate kuthibiti jawabu katika moyo wake baada ya kuwa ameshindwa kujibu, basi inapendeza kwa mlinganiaji achague njia ambazo zitaamsha hamasa, na zitachangamsha akili, na zitavuta usikivu na ufahamu wa karibu.

  4. sio aibu kwa mwanadamu kuto juwa kitu chochote katika mambo ya kidunia au kidini, hakukosea Mua’dh (r.a)- na yeye ni mjuzi wa watu kwa yaliyo halali na haramu- kwa kusema juu ya jambo asilolijuwa: “Mwenyezi Mungu ndio mjuzi zaidi” basi jiepuashe kutoa fat,wa (jawabu) katika dini, jiepushe kujibu maswali ya dini pasina elimu kwa kiburi au haya-aibu-:

    “ Wala msifuate njia za shetani hakika yeye kwenu ni adui wa wazi (168) si vinginevyo shetani anakuamrisheni mabaya na machafu na kumsemea Mwenyezi Mungu yale msiyopyajuwa”

    [al-baqarat:168-169].

    “Msiseme kwa ndimi zenu uongo kwamba hili ni halali na hili ni haramu, kwa ajili ya kumzushia Mwenyezi Mungu uongo, hakika ya wenye kumsemea Mwenyezi Mungu uongo hawatafaulu (116) ni starehe ndogo sana ya hapa duniani, na wanayo wao adhabu kali"

    [al-nahli:116,117].

  5. Kila haki unayoitafuta kwa watu au wayoitafuta kwako: Basi fahamu kuwa kunahaki kubwa zaidi ya hiyo, nayo ni haki ya Mwenyezi Mungu Mtukufu juu yako, pia ni haki kubwa zaidi kuliko idadi ya kila neema zake kwako, basi likumbuke hilo, na yawe maisha yako yamefungamana nayo:

    “ Sema ewe Muhammad, hakika sala yangu, na kuchinja kwangu, na uzima wangu, na kifo changu, ni kwa ajili ya Mola wa viumbe wote (162) hana mshirika na nimeamrishwa kufanya hayo na mimi ni wa mwanzo kunyenyekea "

    [al-an’am:162,163]

  6. Mwenyezi Mungu anahitaji kutoka kwako usimshirikishe na chochote, yaani: kituchochote kama unavyo jiepusha kufanya ushirikina mkubwa, kama kuabudu masanamu, kuomba msaada kwa nyota na kutafuta ukati kwa maneno yasiyofaa, hivyo hivyo ndio ujiepushe na kufanya ushirikina mdogo, kama kuapa kwa viumbe, hata akiwa kiumbe huyo ni Mtume (s.a.w), na kuweka azima-hirizi- ambazo zinaondosha kijicho kwa madai yao, au kumshirikisha Mwenyezi Mungu kwa kusali vizuri kwa kutaka watu wakuone, na mfano wa hayo . Na yamepokelewa maneno katika hadithi al-qudsiy: “Mimi ninajitosheleza na washirika katika kunishirikisha, mwenye kutenda wema wowote akamshirikisha pamoja namimi mwingine asiyekuwa mimi, nitamwacha na ushirikina wake” [6] .

  7. Ulinde moyo wako, na upambane na kila shirki utayo pambana nayo moyo wako, na chukuwa bishara njema ya kheri, imekuja katika hadithi: “Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu, atamtoa mtu katika ummati wangu, kwenye mkusanyiko wa watu wote siku ya malipo, kisha atamfunulia vitabu tisini na tisa [ yaani vya madhambi], na kila kitabu ni mfano wa kikomo cha macho, kisha atasema Mwenyezi Mungu: Je, unakanusha chochote katika hiki kitabu? Je, wamekudhulumu waandishi na wadhibiti wangu? Basi atasema: Hapana ewe Mola wangu! Atasema Mwenyezi Mungu: Je unao udhuru wowote? atajibu kwa kusema: Hapana ewe Mola wangu, atasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: Ni kweli kabisa, hakika wewe unao wema kwetu, na kwa hakika leo hakuna kudhulumiwa, basi kitakuja kitambulisho kimeandikwa: Ninakiri kwa moyo na ninatamka kwa ulimi ya kwamba hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu peke yake, na ninakiri ya kwamba Nabii Muhammad ni mja wake nani Mtume wake, atasema Allah kumwambia mtu huyo: pima uzito wako, atasema Yule mtu: Ewe mola wangu wapi na wapi kitambulisho hiki na hivi vitabu! akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: Hakika wewe hutadhulumiwa leo, akasema: vitawekwa vitabu- vya madhambi- katika sahani ya mzani na kitambulisho kitawekwa katika sahani nyingine, vikawa vyepesi vitabu vya madhambi na kitambulisho kikawa kizito, hakiwezi kuwa kizito pamoja na jina la Mwenyezi Mungu kitu chochote” [7] .

  8. Hadithi za kutoa ruhusa juu ya kitu Fulani huwa hazienezwi kwa watu wote, ili ufahamu wao usije kukosa makusudio, na hakika Mua’dh aliisikia hiyo ruhusa lakini, ikawa sababu ya kumwongezea bidii katika ibada na woga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, lakini mtu ambaye hajafikia daraja lake kiibada, haiaminiki kwa kupunguza ibada kwa uvivu na kubweteka juu ya anayoyafahamu katika habari.[8] Na haya yanakaribiana kabisa na maneno ya ibn masoud (r.a): “ Wewe huwasimulii watu maneno ambayo upeo wao haujayafikia isipokuwa itakuwa ni mtihani kwa baadhi yao[9] .

Marejeo

  1. Kitabu, Majmuu’ al-Fatawa (10/149, 150).
  2. Kitabu, Fath al-Bari cha Ibn Hajar (11/339).
  3. “Al-Kawthar Al-Jari katika Riyadh Ahadith Al-Bukhari” cha Al-Kurani (5/438).
  4. Sahihi Muslim (93), kutoka kwa Jabir bin Abdullah, Mungu amuwiye radhi.
  5. Almufhim katika mukhtasari wa Muslim wa al-Qurtubi (1/290)
  6. Sahihi Muslim (2985) kutoka kwa Abu Hurairah, Mungu amuwiye radhi.
  7. Sunani Al-Tirmidhiy (2639) na Ibn Majah (4300).
  8. Fath al-Bari cha Ibn Hajar (340/11).
  9. Tazama: Sahihi Muslim baada ya Hadithi Na. (5).

Miradi ya Hadithi