عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضى الله عنه، أَنَّ النَّبِيَّ ، قَالَ: «نَارُكُمْ هَذِهِ الَّتِي يُوقِدُ ابْنُ آدَمَ جُزْءٌ مِنْ سَبْعِينَ جُزْءًا مِنْ حَرِّ جَهَنَّمَ» قَالُوا: وَاللهِ إِنْ كَانَتْ لَكَافِيَةً يَا رَسُولَ اللهِ! قَالَ: «فَإِنَّهَا فُضِّلَتْ عَلَيْهَا بِتِسْعَةٍ وَسِتِّينَ جُزْءًا، كُلُّهَا مِثْلُ حَرِّهَا».

Kutoka kwa Abu Hurayrah radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie kwamba Mtume Rehma na Amani zimshukie amesema:

“Huu moto wenu anao uwasha mwana wa Adam ni sehemu moja katika sehemu sabini za joto la Jahannamu. Wakasema: ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Wallahi, huu moto wa Duniani ulikuwa unatosha kabisa kwa kuadhibu  kutokana na ukali wake,  Akasema: “Hakika moto wa Jahannamu ukali wake umeongezwa juu yake sehemu sitini na tisa, na kila sehemu moja ni sawa na joto la moto wa dunia nzima.”

  1. Mtume Rehma na Amani zimshukie analinganisha moto wa dunia na moto wa Akhera. Ametaja kuwa joto la moto wanaotumia watu hapa duniani ni sehemu moja tu ya moto wa Akhera ambao Mwenyezi Mungu Mtukufu amewaandalia makafiri na wakosefu.

  2. Habari hiyo ikawa ni nzito sana kwa Maswahaba ,na wakajibu kuwa lau moto wa Akhera ungekuwa kama moto wa dunia katika kuungua na joto, ungetosha kuwa adhabu, na ungetosha kumzuia mtu kutumbukia katika maasi na kuacha maamrisho; hayo ni kwasababu huu moto wa duniani unao uwezo wa kuteketeza  wanadamu, wanyama, mimea na vitu vingine visivyo hai.

  3. Mtume Rehema na Amani zimshukie akasisitiza kuwa moto wa Akhera ni mkali mara 69 kuliko huo moto ambao walimwengu wameuzoea na kuonja joto lake, ili iwe nyongeza ya Adhabu katika kuwaadhibu makafiri na wakosefu.

Mafunzo

  1. Ni juu ya kila Mzungumzaji – kuanzia mzazi, mlinganiaji, mwalimu na wengine - kuwasilisha vyema maana anazotaka, kwa kutumia mifano, nambari au hata mambo mengine yanayoleta ufahamu na taswira nzuri.

  2. Kuwakumbusha watu kwa kutaja neema za peponi na kubainisha Adhabu za motoni ni miongoni mwa mawaidha mengi sana yaliyotajwa ndani ya Qur’ani Tukufu, inapendeza zaidi kuwepo kwa mawaidha ya aina hiyo katika misikiti, majumbani, vikao na hata katika vyombo vya habari.

  3. Moto unaoongezeka mara sabini juu ya moto wa dunia hii kwa ukali, ni bora kuukimbia moto huo, na kuzidisha mema ambayo yatamweka mbali na Moto. Ushindi wa kweli unapatikana kwa kuokoka kutokana na Moto na kuingia Peponi. Mwenyezi Mungu amesema:

    “Basi mwenye kuondolewa Motoni na akaingizwa Peponi atakuwa ndio mshindi”

    [Al Imran: 185].

  4. Kuchukuwa Tahadhari kutokana na moto wa dunia ni jambo ambalo liko kisheria, na Mtume Rehema na amani ziwe juu yake alitoa maelekezo hayo, hata namana ya kuzima taa ndogo ili isije ikaunguza nyumba. Ni akili sahihi kuchunga na kuondosha kila sababu ambayo inaweza kusababisha mlipuko wa moto, japokuwa inafaa kisheria kuutumia moto, hivyo kujiepusha na moto wa siku ya kiyama ndio bora zaidi.

  5. Ni ushujaa na ni katika matendo mema kuwaokoa watu na moto wa dunia hii na kuuzima, na wanaofanya hivyo hupongezwa, hivyo walinganiaji wanaowaita watu katika njia ya Mwenyezi Mungu na wale wanaotoa nasaha wameepushwa na moto mkali zaidi, hivyo kuwapongeza watu hawa ni jambo kubwa na tukufu sana na ni wajibu kuthamini juhudi zao.

  6. Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, alikuwa akiomba ulinzi wa Mwenyezi Mungu kutokana na joto la Moto wa Jahannam. Kutoka kwa Abu Hurairah Mwenyezi Mungu awe radhi naye amesema: Nimemsikia Abal-Qasim rehema na amani ziwe juu yake anasema katika sala yake: “Ewe Mola wangu, najikinga kwako kutokana na fitna za kaburi, Na kutokana na majaribu ya Mpinga Kristo, na kutokana na mitihani ya uhai na kifo, na kutokana na joto la Moto wa Jahannam”[1]; Ikiwa Mtume, Rehema na Amani zimshukie, anaomba ulinzi kutokana na Jahannamu na yeye ndiye alihifadhika na kutenda dhambi pia amesamehewa madhambi yake yaliyotangulia na yajayo, basi vipi sisi?! Ni lazima kwa kila Muislamu kutopuuza adhabu ya Moto.

  7. Mshairi alisema:

Na chukua hifadhi imara kwa kumcha Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema = kwa ajili ya siku ambayo Jahannamu itaonekana.

Na daraja litajengwa juu ya Jahannam = basi wapo watakaoangukia humo, watakao hangaika na wengine kusalimika

Na Mola wa walimwengu itatimia ahadi yake = ataamua baina ya waja na kutoa hukumu

Na Mola wako Mlezi atairudisha haki ya aliyedhulumiwa = ubaya ulioje kwa mtu mwenye kuwadhulumu watu.

Marejeo

  1. An-Nasa’i (5520).


Miradi ya Hadithi