Maneno haya ya Mtume ndio miongoni mwa misingi ya uislamu, na nimiongoni mwa maneno yake mafupi sana lakini yamekusanya maana pana sana:
1. Hivyo ameeleza kwamba mwanadamu zikipatikana kwake sifa tatu ataipata ladha ya imani, yaani ni ladha ambayo ataihisi moyoni mwake kama ambavyo mtu anaihisi ladha ya chakula, na hii ni kama maneno ya Mtume : “ Ameonja ladha ya imani mtu ambaye ataridhia kuwa Mwenyezi Mungu ndio mola wake, na uislamu ndio dini yake, na Mtume Muhammad ndio Mtume wake” [1] na hayo ni kama mfano wa yale anayoyapata muumini kwa kukunjuka kifua chake, na kuingia nuru kifuani mwake kwa kumtambua Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kumtambua Mtume wake , [2] na kuipata ladha ya utiifu kwa Mwenyezi Mungu, na kuvumilia matatizo na shida katika kumridhisha Mwenyezi Mungu Mtukufu na na Mtume wake, na kuyafadhilisha hayo juu ya thamani ya dunia [3]. “ na imani ndio chakula cha nyoyo na nguvu zake kama ilivyo chakula na kinywaji ni chakula cha viwiliwili na nguvu zake, kama ambavyo mwili haupati ladha ya chakula na kinywaji isipokua wakati wa afya nzuri ,basi mtu akiwa mgonjwa hapati ladha ya kitu chochote kinacho mnufaisha kutokana na maradhi, bali anaweza kuhitajia kitu ambacho kinaweza kumdhuru au au akahitaji kitu ambacho hakina ladha, kwa sababu ya kuzidiwa na maradhi, basi hiyo ndio hali ilivyo kwenye moyo, moyo haupati ladha ya imani kutoka na maradhi yake na majanga yake, kwani moyo unaposalimika kutokana na maradhi ya pumbao lenye kumpoteza mtu , na matamanio yaliyo haramishwa, hapo ndipo moyo unapata ladha ya imani, na muda wowote moyo ukipatwa na maradhi, haupati ladha nzuri ya imani; bali anaweza kutafuta ladha kwa vitu ambavyo vinaweza kuwa sababu ya kuangamia kwake katika pumbao na maasi; kwa hakika laiti ingekamilika imani yake basi angepata ladha hiyo ya imani, basi akatosheka nayo kuliko kutafuta ladha kwa kufanya maasi” [4].
2. Ama sifa ya kwanza: katika sifa hizo ni: “ Awe Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapendeza kwake zaidi kuliko wengine wasiokuwa hao” na makusudio ya kumpenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake: Ni hisia anazozijua mwanadamu moyoni mwake, na inampatia wingi wa kumtaja kipenzi chake, na kumtamania, na kufanya anayoyapenda, na kujiepusha na anayoyachukia, na yanaendelea kuongezeka mapenzi mpaka kufikia hali ya kumtanguliza juu ya kila mpenzi mwingine, bali yanapelekea kutoa kipaumbele kwa kutenda yale anayo yapenda mpenzi wake, na japo akiwa kinyume na matamanio ya nafsi.
Na haya mapenzi (ya kumpenda Mwenyezimungu na Mtume wake) ni wajibu yawe ni yenye kupewa kipaumbele zaidi katika moyo wa kila muislamu juu ya kila anaependwa, na kama sio hivyo basi mtu huyo atakua amejiingiza katika kupata chuki za Mwenyezi Mungu na adhabu zake:
“Sema ewe Muhammad kuwaambia watu wako,ikiwa mtawaona baba zenu, na watoto zenu ,na ndugu zenu, na wake zenu, na jamaa zenu, na biashara ambazo mnahofia kupata hasara, na majumba mnayoyapenda, (mkayaona hayo) kuwa ndio bora zaidi kuliko kumpenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake (s.a.w) na kupigana jihadi katika njia yake, basi subirini adhabu kali mtakayoipata kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu waovu (wasiofuata maamrisho yake” .
Na amesema Mtume rehma na amani ziwe juu yake: “hawi na imani kamili mmoja wenu, mpaka niwe mimi napendeka kwake kuliko baba yake, na watoto zake, na watu wote” [5].
3.Ama sifa ya pili: ni kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ndio awe mwamuzi wake katika kupenda kwake mwanadamu, basi mtu ampende mtu si kwa kitu kingine isipokuwa ni kwamba Mwenyezi Mungu anampenda mtu huyo au ameamrisha kumpenda mtu huyo. Na imekuja katika maneno ya Mtume , “Hakika imani iliyoimarika hasahasa ni kupenda kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na kuchukia kwa ajili yake” [6]. Mtu haachi kuendelea kujisalimisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu mpaka anaku Mwenyezi Mungu ndio mwamuzi juu yake katika kila mapenzi, kama asemavyo
“Kwa hakika imekuwa kwenu ni kiigizo kizuri, kwa Nabii Ibrahim na waliokuwa pamoja naye,waliposema kuwaambia watu wao (makafiri) sisi tuko mbali nanyi na vyote mnavyo viabudu kinyume na Mwenyezi Mungu Mtukufu, na umekuwa wazi uadui na chuki za milele kati yetu na nyinyi, mpaka muwe waumini juu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu peke yake”.
Na imekuja katika hadithi za Mtume : “Mtu yeyote atakae penda kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na akachukia kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, nakatoa kwa ajili yake, na akajizuia kutoa kwa ajili yake, hakika atakuwa ameikamilisha imani” [7].
4.Na sifa ya tatu: ni kuchukia kuingia katika ukafiri na maasi- sawasawa aliingia katika hivyo viwili hapo kabla au laa- hakika mwenye imani ya kweli na akafungamana na kumpenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake inakuwa kuacha kwake neema ya imani ni moto anaouchukia, kama ambavyo hapendi kuingia motoni [8].
Na kiasi cha wajibu cha kuchukia madhambi ni kuitoa nafsi katika madhambi na kujiweka mbali nayo, na kuweka maazimio ya kutorudia tena; kwa kujua chuki za Mwenyezi Mungu dhidi yake, ama kuyumba kimaumbile na kuingia kwenye madhambi bila kuwepo hali ya kuyapenda au kuyafanya bahati mbaya; hatoadhibiwa. Kwa hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu amemsifu mwenye kuikataza nafsi yake kutokana na matamanio, hilo linajulisha kwamba matamanio yanaweza kumyumbisha mtu na kumpelekea kufanya kitu ambacho kimezuiliwa kisheria, lakini muumini halisi huikataza nafsi yake na yote hayo
MAFUNDISHO
1.Alikwenda mama suleym na mwanae anas ibn malik kwa Mtume ili akawe mtumishi wake, na hiyo ni dalili kubwa juu ya mapenzi ya dhati kwa Mtume Muhammad , kwa kuwa mtoto wake ndio alikuwa tulizo la jicho lake, lakini pia ni mtu huru na sio mtumwa, na hakumtumikia kwa kutaka mali, sasa sisi ni kitu gani ambacho tumekitanguliza kwa ajili ya dini ya Mtume Muhammad rehma na amani ziwe juu yake, na maneno yake na sunna zake?
2.Alitumia Mtume katika maneno yake njia za kutamanisha na kumvutia mtu na kumzindua.Bbasi akaanza mazungumzo kwa kutaja mambo tena kwa idadi maalum,ili msikilizaji awe makini katika kuvidhibiti, kama ilivyokuja katika tamko “ utamu na ladha” ili apupie mwanadamu kudhibiti vitu hivyo kwa ajili ya kuipata hiyo ladha, basi ni juu ya walinganiaji na makhatwibu na watoa mawaidha wapupie kufuata njia za kida’wah zenye kuvutia.
3.Kila unapoona nafsi yako inapunguz\a kufanya ibada, basi ingiza katika moyo wako mapenzi ya kumpenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake , kutoka kwa Anasi hakika mtu mmoja alimuuliza Mtume kunako qiyama (siku ya malipo), basi akasema: “umeiandalia nini siku hiyo”? Akasema Yule mtu: sijaandaa chochote lakini Mimi ninampenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake , basi akasema Mtume rehma na amani ziwe juu yake: “wewe utakuwa siku hiyo na Yule uliempenda”. Amesema Anasi: Hatukuwahi kufurahia jambo lolote kama tulivo furahia, maneno ya Mtume rehma Na amani ziwe juu yake aliposema “wewe utakuwa siku hiyo Na Yule uliempenda”. Akasema Anasi : mimi ninampenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na ninampenda abubakar na Omari , basi ninatarajia kuwa pamoja nao, hata kama sikufanya ibada kubwa kama wao [9] .
4.Kila usikiapo kitendo cha mpenzi kwa mpenzi wake, basi wewe uwe na mapenzi ya juu zaidi kuliko hayo pale yanapo fungamana na Mwenyazi Mungu mtukufu na Mtume wake , na mapenzi hayo yako katika ngazi tofauti, katika mapenzi hayo ni yale yanayopatika kwa kutekeleza yaliyo wajibu, na kujiepusha na kufanya yaliyo katazwa, na katika hayo yapo yanapatikana kwa kutekeleza sunnat za Mtume Muhammad rehma na amani ziwe juu yake, na kujiepusha kuingia katika mambo ya shubuha.
5.Sasa tujifunze na tuwafunze wanaotuzunguka namna ya kukuza na kuyaboresha katika nyoyo zetu mapenzi ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake , basi mwenye kukaa na kufikiri namna ya kuyapata mapenzi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na kuyatambua majina yake na sifa zake na ukamilifu wa kazi zake allah mtukufu, na akachunguza kwa umakini uzuri wa matendo ya Mwenyezi Mungu kwake, na kuikumbusha nafsi ukubwa wa neema za Mwenyezi Mungu, na ukubwa wa rehma zake, pamoja na ukubwa wa madhambi, na mfano wake huambiwa katika kumpenda Mtume wa Mwenyezi ,Mungukwa ufahamu wake rehma na amani ziwe juu yake, na kusimama juu ya mambo mazuri na ukubwa wa jihadi yake Mtume katika njia ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kuwa yeye ndio sababu ya kuongoka kwetu kwenye njia sahihi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na yasiyo kuwa hayo.
6.Mwanadamu anaweza kuiathiri nafsi yake ili ipende kitu au ikichukie,basi ichunguze nafsi yako na upambane nayo mpaka ifadhilishe mapenzi ya Mtume yawe juu ya kila kitu, hakika Mtume alishika mkono wa omari , akasema omari kumwambia Mtume rehma na amani ziwe juu yake, ewe Mtume wa allah,naapa kwa Mwenyezi Mungu wewe unapendeza kwangu kuliko kila kitu isipokuwa nafsi yangu pekee,akasema Mtume : “ hapana, ninaapa kwa Yule ambaye nafsi yangu iko mikononi mwake, nipendeze kwako mpaka niwe zaidi ya nafsi yako” akasema omari: Hakika sasa hivi naaapa kwa jina la Allah, wewe –Mtume- unapendeza kwangu kuliko hata nafsi yangu, hapo akasema Mtume rehma na amani ziwe juu yake: “sasa hivi ewe omari- imani yako imekamilika-kuliko hapo kabla” [10]
7.Utakapo mpenda muislamu basi dhihirisha alama za upendo huo kwa kiasi itavyo wezekana kwa kila mmoja, kama kukaa nae, na kutembeleana, na kupeana, kwani “mtu mmoja alimtembelea ndugu yake kijiji kingine, basi, Mwenyezi Mungu akamtumia -katika mwendo wake wa safari hiyo- Malaika, alipomuendea, alisema Malaika kumwambia Yule mtu: unakwenda wapi? Akajibu: nimekuja kumtembelea ndugu yangu katika kijiji hiki, akasema malaika: je, kuna neema-mali- unaitaka kutoka kwake? Akajibu: hapana, isipokuwa mimi ninampenda tu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, akasema malaika: Basi hakika mimi ni mjumbe kutoka kwa Mwenyezi Mungu kuja kwako, hakika Mwenyezi Mungu amekupenda kama ulivyopenda kwa ajili yake” [11].
8.Wakati wowote utakapo mpenda rafiki kwa ajili ya Mwenyezi Mungu basi hifadhi upendo huo uwe maalum kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwani mwenye kumpenda mtu kwa lengo lingine yatakatika mapenzi hayo pale tu lengo litakapo katika na kukamilika, au kukata tamaa ya lengo hilo,[12] na ukamilifu wa kumpenda Mwenyezi Mungu: yasizidi kwa kufanya wema na hayapungui kwa kufanya uovu. [13]
9.Izoweshe nafsi yako kuyakataa maasi, na kuyachukia chuki ambayo itapelekea kuto kuyaendea, na uwe na tahadhari kuyapenda maasi katika nafsi yako, au kuyadhania kwa sura nzuri katika nafsi, kwani yaliyofichikana ndio funguo za matashi, na matashi ndio funguo za matendo.
10.Amesema Mshairi:
Unamuasi mola haliyakuwa unadhirisha kumpenda = hili haliwezekani katu katika vipimo na mizani,
Laiti ingekuwa upendo wako ni wa kweli basi ungemtii = hakika mwenye kupenda kwa ampendae ni mtiifu.
Kila siku zinakuijia neema = kutoka kwake na wewe unapoteza shukrani zake.
11.Amesema abuu qaysi al-answariy akitaja ujio wa Mtume kwao mjini madina: [14]
Aliishi kwa maqureysh kiasi cha miaka kumi = akiwakumbusha nakuwaonya laiti angekutana na kipenzi mwenye kujali
Zama alipokuja kwetu na yakatulia malengo kwake = na akawa mwenye furaha kwa uzuri wa ridhaa
Tulimpatia mali katika mali zetu za halali = na nafsi zetu wakati wa vita na amani.
Tunamchukia mwenye kufanya uadui katika watu wote = hata kama atakuwa ni rafiki mzuri.
Marejeo
- Muslim (34), kutoka kwa Al-Abbas bin Abdul Muttalib, Mungu amuwiye radhi.
- "almufhim lamaa 'ashakal kwa Kufupisha wa Kitabu cha Muslim” cha Abu Al-Abbas Al-Qurtubi (1/ 210).
- “Al-Minhaj katika sherh ya Sahih Muslim Bin Al-Hajjaj” cha Al-Nawawi (2/13).
- Fath al-Bari cha Ibn Rajab (1/50-51)
- .Sahihi Al-Bukhari (15) na Muslim (44), kutoka kwa Anas bin Malik, Mungu amuwiye radhi
- .Ahmad No (18524) kutoka kwa Al-Baraa bin Azib, Mungu amuwiye radhi
- .Abu Dawood Na. (4681), kutoka kwa Abu Umamah Al-Bahili.“Sharh Riyadh as-Salihin” cha Ibn Uthaymiyn (3/260)
- .Fath al-Bari, ufafanuzi wa Sahih al-Bukhari, cha Ibn Rajab al-Hanbali (1/58)
- .Sahihi Al-Bukhari (3688) na Sahihi Muslim (2639)
- .Sahihi Al-Bukhari (6632)
- .Sahihi Muslim (2567)
- .Tazama: “Al-Mufhim limaa ashkil katika kufupisha Kitabu cha Imamu Muslim” cha Abu Al-Abbas Al-Qurtubi (1/214)
- .Tazama: Fath Al-Bari, ufafanuzi wa Sahih Al-Bukhari” cha Ibn Hajar Al-Asqalani (1/62)
- . Tazama: sirat cha Ibn Hisham (1/512).