عن أبي سُليمانَ مالكِ بنِ الحُوَيْرثِ رضي الله عنه، قال:أَتَينا النبيَّﷺ ونحن شَبَبةٌ مُتقارِبون، فأقمْنا عنده عِشرين ليلةً، فظنَّ أنَّا اشتَقْنا أهْلَنا، وسألَنا عمَّن ترَكْنا في أهلنا، فأخبرناه، وكان رفيقًا رحيمًا، فقال: «ارْجِعوا إلى أهلِيكم،فعلِّموهم ومُروهم،وصلُّوا كما رأيتموني أُصلِّي،وإذا حضَرتِ الصلاةُ، فلْيُؤذِّنْ لكم أحدُكم، ثم لِيَؤُمَّكم أكبَرُكم»

Kutoka kwa Abu Sulaiman Malik bin Al-Huwairith, Mwenyezi Mungu amuwie radhi, amesema:

1. Tulikuja kwa Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake) tukiwa vijana tukikaribiana, tukakaa kwake siku ishirini, akadhani tumetamani familia zetu, akatuuliza kuhusu tuliowaacha katika familia zetu, tukamwambia. 2. na Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake) Alikuwa ni mpole mwenye huruma, akasema: “Rudini kwa ahali zenu. 3. Wafundisheni na waelekezeni. 4. na swalini kama mlivyoniona nikiswali, 5. Na ukifika wakati wa Swala, mmoja wenu aadhini, kisha awaongoze mkubwa wenu”

1.   Malik bin Al-Hawairith, Mwenyezi Mungu amuwie radhi , akiwa na kundi la maswahaba zake kutoka Bani Al-Layth walimtembelea Mtume, rehema na amani ziwe juu yake. Wote walikuwa ni vijana waliokaribiana katika umri, walikaa kwa Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake) kwa muda wa siku ishirini, wakijifunza na kuifahamu Dini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake) alipohisi kuwa wamezitamani familia zao, akawauliza kama waliacha jamaa zao, wakamwambia waliwaacha katika jamaa zao.

2. Walipomwambia, akawaamrisha warejee kwao, na hiyo ni kwa sababu ya  upole na huruma ya Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake) kwa Waumini, kwani Mwenyezi Mungu alishasema kuhusu hilo. ndani yake:

" Hakika amekwisha kujieni Mtume kutokana na nyinyi wenyewe; yanamhuzunisha yanayo kutaabisheni; anakuhangaikieni sana. Kwa Waumini ni mpole na mwenye huruma"  . 128

[At-Tawbah: 128].

Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake) aliwaamrisha warudi kwenye familia zao, Kwa sababu hiyo ilikuwa baada ya ufunguzi wa Makka; kwani Kuhama kulikatishwa na ufunguzi wa Makka; Kwa kauli yake aliposema : “Hakuna kuhama baada ya ufunguzi wa makkah”, [1]kwa hiyo makazi ya Madina yakawa ni ya hiari, kwa aliyetaka alibaki, na anayetaka alirejea kwa watu wake baada ya kujifunza anachohitaji kutoka katika elimu na dini, na kufundisha watu wake.[2]Aliwaruhusu warudi na kuwaamuru wafanye hivyo, Kwa sababu alijua kuwa wamejifunza yale yanayowatosheleza katika mambo ya dini yao ya fiqh na tauhidi, la sivyo, asingewaacha warudi kwenye familia zao achilia mbali kuwaamuru wafundishe.

3. Ndio maana akawaamrisha wawafundishe watu wao yale waliyowafundisha katika Dini ya Mwenyezi Mungu, Bali akawaambia kuwa elimu peke yake haitoshi, basi kila mmoja anatakiwa kuamrisha familia yake na kuwachunga, kwani wao ni wenye kuulizwa na kuhesabiwa kwa familia zao,.” Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

"Na waamrishe watu wako kusali, na uendelee mwenyewe kwa hayo."

[Twaha: 132].. ”

    Na Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake) amesema: “Kila mmoja wenu ni mchunga na anawajibika kwa kundi lake.”[3]  kama ilivyo vile kufundisha ni wajibu, ndivyo ilivyo wajibu kufanyia kazi elimu.[4]

4. Kisha Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake) akaweka kanuni pana katika dini na hukumu zake, nayo ni kumfuata Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake) na kumfuata katika swala na namna zake na hukumu zake, na yale yanayosemwa ndani yake, na yanayoibatilisha, na yanayolazimu sijda ya kusahau; kwani hakika Matendo ya Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, ni maelezo yanayobainisha kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu aliyoitaja kwa ujumla katika Qur’ani Tukufu; kwani Aayah za Qur-aan hazikuja zikifafanua kwa upana hukumu za swala, idadi ya rakaa zake, nyakati zake, nguzo zake, sunna na sura zake. Bali ilikuja zikiamrisha swala ihifadhiwe kwa muda wake, Zikiacha  kauli za Mtume na matendo yake yabainishe kwa upana na uwazi, na ndio maana yeye, amani iwe juu yake, alisema: “Swalini kama mlivyoniona mimi nikiswali.”Vivyo hivyo inatumika katika sheria zote na hukumu nyinginezo, Katika Hijja, Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake) anasema: “Hebu chukueni ibada zenu, kwani sijui nitahiji baada ya Hija hii” [5]na Wanazuoni wameafikiana kwamba ikiwa vitendo vya Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake) ni ufafanizi kwa jambo lilokuja kwa jumla bila ufafanuzi, kama vile kuswali, kufunga na kuhiji, basi matendo hayo yatachukuliwa kama ni wajibu, isipokuwa ziwepo dalili mahususi zinaonyesha kuwa si wajibu[6]Na wajibu huu ni juu ya Ummah wote, kwa sharti ithibitike kuwa Mtume, (Rehma na amani ziwe juu yake) aliendelea na kitendo hicho maalum, basi itakuwa ni wajibu kwa Ummah wake, Ama kile ambacho hakijathibitishwa kuendelea nacho, basi si wajibu.[7]

5. Kisha Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake) akawausia itakapofika wakati wa swala, mmoja wao aadhini, na mkubwa wao awaswalishe.Na asili katika uimamu ni kwamba anaesoma vizuri Qur'ani ndo anapaswa kuwasalisha, kama ilivyo katika hadithi ya Abu Masoud al-Ansari, Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake  kwamba Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, amesema: awaswalishe watu Yule anaejua kusoma vizuri zaidi Kitabu cha Mwenyezi Mungu kuliko wote, basi ikiwa wako sawa katika kusoma, basi mjuzi zaidi yao katika Sunnah, na ikiwa ni sawa katika Sunnah, basi aliewatangulia katika kuhama, na ikiwa ni sawa katika kuhama, basi aliewatangulia katika kuingia kwenye uislamu[8],Amr bin Salamah, Mwenyezi Mungu amrehemu, aliwaswalisha watu wake wakati wa Mtume Rehema na amani ziwe juu yake akiwa na umri wa miaka sita. Kwa sababu alikuwa vizuri katika usomaji wa qur`an kuliko wote,[9] Bali Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake) aliwaamrisha kuwatangulia wakubwa wao, kwa sababu  alijua kuwa kisomo chao kinakaribiana; kwa Ushahidi wa kauli yake katika riwaya ya Muslim: “Walikuwa wanakaribiana katika kusoma”[10] na waliingia katika Uislamu wakati mmoja, mara nyingi watu wa namna hiyo Kuna uwezekano mkubwa kwamba usomaji wao na elimu ya Sunnah ni sawa, kwahiyo ndio maaana akatangulizwa mkubwa  wao.

MAFUNDISHO :

1. Katika hii hadithi kuna ubainifu kuwa Maswahaba Mwenyezi Mungu awe radhi nao, walijali sana swala la kutafuta elimu na kujifunza hukumu mbalimbali za kisheria, na kwamba waliacha familia zao na makazi yao kwa ajili hiyo, na hii ni kutokana na yale yaliyotua ndani ya nafsi zao juu ya fadhila na ukubwa Wake, hivyo basi mtu asikose ujira huo, hasa katika zama hizi ambazo kutafuta elimu kumemjia bila ya taabu wala shida za safari.

2.Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake) aliwajali sana vijana na alikuwa na shauku ya kuwaelimisha kisha kuwatuma kama mabalozi na walinganizi kwa watu wao; kwa sababu Vijana ndio nguzo ya ummah huu na chanzo cha maendeleo yake, hivyo basi Maslahi yao lazima yaelekezwe kwenye kazi, na ulinganiaji na kujenga ummah.

3.Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake) alielewa hali za kisaikolojia za vijana na akaelewa mahitaji yao ya kihisia, na kwa sababu hiyo akawaruhusu warudi kwenye familia zao, hivyo basi inampasa mlinganiaji au mwalimu kuchunga mahitaji ya vijana na kuzingatia hali zao na kuchukuliwa tahadhari maalumu kwa ajili yao.

4.mlinganiaji, na mwalimu, na mlezi lazima awe mpole mwenye huruma, ambaye ulinganiaji wake haupingani na mahitaji ya lazima ya watu, bali awahurumie kwa kadiri inavyowezekana, na ajitahidi kutumia nyakati za uchangamfu wao katika yale yanayowanufaisha, na kuwapa faraja na nafasi inayoendana na miili na roho zao.

5.Miongoni mwa busara za mlinganiaji na mlezi ni kwamba asimtwike mtu yeyote kile asichoweza kustahimili, bali azingatie nguvu na uwezo wake wa kutekeleza yale aliyoamrisha kidogo kidogo.

6. inamampasa Mtu abaki na familia yake kadiri awezavyo, na asiwe mbali nao, ndio maana Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake) alimuamuru msafiri pale atakapomaliza haja yake arudi katika familia yake .[11] Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake) amehusia katika hadithi hii na katika hadithi nyinginezo kufikisha ujumbe wa dini hii na kueneza ulinganiaji wake, na katika hilo kuna kauli ya Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake) isemayo “fikisheni kwa niaba yangu hata kwa ayah moja”[12]; hivyo basi Mwenye kulingania ni mfikishaji kutoka kwa  Mwenyezi Mungu na Mtume wake (Rehma na amani ziwe juu yake) anakuwa kwa watu amesimama katika cheo cha Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake) akiwalingania watu kwenye kheri na kuwakataza maovu na kuwaeleza sheria za kidini na kuwafahamisha hukumu zake.  Je Nani asingependa kuwa katika daraja hilo?!

8.Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake) ameeleza kuwa kulingania kunahitajia amri na subira katika utekelezaji, na si kubainisha maamrisho na makatazo tu, kwani kiasi Mtume rehema na amani ziwe juu yake alivumilia ili kufikisha sheria za Mwenyezi Mungu,?! Hivyo basi walinganiaji na wanachuoni wanapaswa kuwa na subira na na kuhimizana katika hilo ili kutekeleza sheria ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.

9. Ubainifu wa hukumu za Sheria umekabidhiwa kwa Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake) peke yake, si kwa maneno ya watu, wala si kwa kutumia akili tu, na wala si kwa matamanio; kwani Ibada lazima itegemee matendo na maneno ya Mtume rehema na amani ziwe juu yake, hakuna kuzidisha wala kupunguza katika yale aliyoyawekea sheria.

10. Kumfuata Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake) katika Sunnah zake ndio njia ya uzima na uwongofu; kwani Kupitia kwayo Muislamu anajua namna sahihi ya swala, na muda wake, na hukumu zake, na nguzo zake na sifa zake, na akaweza kudhibiti hukumu za ibada nyinginezo, kama zaka, saumu, kuhiji na nyenginezo. Na lau Muislamu angeliacha kufuata Sunnah za Mtume (saw), basi atabaki ameduwaa na kupotea njia.

11. Imejumuishwa katika kumfuata Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake) katika swala ni kumfuata katika kukubali kutumia ruhusa za kisheria, hivyo basi katika kumuiga Mtume vizuri ni pale mgonjwa anaposali kwa kukaa au kwa kuegemea kulingana na hali yake, na msafiri na mgonjwa wafungue saumu ikiwa watapata madhara kutokana na saumu hiyo, na msafiri aswali kwa kuunganisha, na ruhusa nyinginezo ambazo alizotumia Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake) wakati wa uhai wake, na akasema: “Mwenyezi Mungu hupenda kutumiwa ruhusa zake kama anavyochukia kuasiwa[13]” 

12. Hadithi hii inaelekeza kumuheshimu mkubwa na kumuweka kataka daraja na hadhi inayomfaa katika mambo yanayozingatiwa kisheria, na hiyo ni wakati ambao haitoleta uvunjaji wa sheria; kwani Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake) alifanya umri kuwa kigezo kuwa imaamu ikiwa watu wako sawa katika vigezo vya uimaamu, kama vile kusoma qur`an vizuri, kuwa na elimu ya sheria, na kutangulia katika Uislamu.

Marejeo

  1. Imepokewa na Al-Bukhari (2783) na Muslim (1353).
  2. Tazama: “Fath al-Bari” cha Ibn Hajar (13/ 236).
  3. Imepokewa na Al-Bukhari (2409) na Muslim (1829).
  4. Tazama: “Sharh Riyadh as-Salihin” cha Ibn Uthaymiyn (4/148).
  5. Imepokewa na Muslim (1297).
  6. Tazama: “Sharh Sahih Al-Bukhari” cha Ibn Battal (10/345), “Riyad Al-Afham fi Sharh Umdat Al-Ahkam” cha Al-Fakhani (2/167).
  7. Tazama: Fath al-Bari cha Ibn Hajar (13/237).
  8. Imepokewa na Muslim (673).
  9. Imepokewa na Al-Bukhari (4302).
  10. Imepokewa na Muslim (674).
  11. “Sharh Riyadh Al-Salihin” cha Ibn Uthaymiyn (4/147).
  12. Imepokewa na Al-Bukhari (3461).
  13. Imepokewa na Ahmad (5866).


Miradi ya Hadithi